Serikali Kuimarisha Uwanja wa Ndege wa Mpanda

Meneja wa Msimamizi wa Bandari ya Kigoma Bw. Morris Mchindiuza (aliyenyoosha mkono) akimwonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (Wa pili kulia) eneo itakapojengwa bandari ya Kalema iliyopo Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi.

 

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (katikati) akitoa maelekezo kwa Meneja wa Kiwanja cha ndege cha Mpanda Seth Lyatuu (kushoto) wakati alipokagua huduma za uwanja huo Mkoani Katavi.

 

SERIKALI imemuagiza Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda kuwasiliana na Kampuni ya Uendelezaji Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KADCO) ili kupata gari la Zimamoto ili ndege za Shirika la ndege Tanzania (ATCL) ziweze kuanzisha safari zake katika Mkoa wa Katavi.
Akizungumza mara baada ya kukagua uwanja huo Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani amesema kwa muda sasa kiwanja hicho kimekuwa kikitumiwa na ndege chache za Shirika la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), hivyo ni wakati sasa kutumika na ndege zetu ili kuboresha huduma za usafiri wa anga Mkoani hapa.
“Kamilisheni mazungumzo na KADCO ili kupata gari la Zimamoto lenye ujazo wa Lita 4,000 litakalokuwa na uwezo wa kukabiliana na majanga ya moto endapo yatatokea, kutakapokuwa na gari hilo uwanjani hapa tutaanzisha safari za ndege za Shirika letu wakati ndege yetu ta tatu itakapowasili,” amesema Eng. Ngonyani.
Aidha, amemtaka meneja wa Uwanja huo wa ndege kuhakikisha anaingiza uwanja huo katika mpango maalum kwa ajili ya ujenzi wa taa kiwanjani hapo ili uwanja huo uweze kutumika kwa mchana na usiku. Eng. Ngonyani ameongeza kuwa azima ya Serikali ni kuhakikisha usafiri wa anga nchini unaimarika kwa kutumia ATCL na mashirika mengine yalipo nchini hivyo kama Serikali imejipanga kuendelea kuboresha miundombinu ya viwanja ili viwe katika viwango vinavyokubalika.
Kwa upande wake Meneja wa Uwanja huo Seneth Lyatuu amemuhakikishia Eng. Ngonyani kuwa changamoto ya kuwa na Gari la zimamoto itatatuliwa mapema ili wakazi wa Mpanda waweze kunufaika na huduma za ATCL na hivyo kuwapa unafuu watumiaji wa usafiri wa anga.
“Kuanza kwa safari za ATCL hapa Mpanda kutawapunguzia gharama wananchi ambao kwa sasa hulazimika kwenda Mwanza au Mbeya ili kupata ndege ya kwenda Dar es Salaam na gharama huwa kubwa,” amesisitiza Lyatuu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Bw. Saleh Mhando amesema kutalete tija na kutafungua fursa ya utalii wa ndani na nnje ya nchi hasa kwa kuwepo na Mbuga ya Katavi ambayo ina vivutio vingi. Katika hatua nyingine Eng. Ngonyani amelipongeza Shirika la Reli Tanzania (TRL) kwa kutekeleza agizo la Serikali la kutumia Mfumo wa kielektroniki katika kudhibiti mapato ambapo shirika hilo limeanza kukatisha tiketi kwa njia hiyo katika stesheni za Mpanda na Tabora.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.