Serikali Kuhakiki Vyama vya Kijamii

Frank Mvungi

Serikali imedhamiria kuanza zoezi la kuhakiki vyama vya kijamii ili kuboresha huduma zinazotolewa na vyama hivyo hapa nchini tangu kuanzishwa kwake.
Hayo ya mesemwa Jijini Dar es salaam na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi Bw. Isack Nantanga wakati wa mkutano na waandishi wa habari .

“Katika kuboresha huduma na usimamizi wa vyama vya kijamii, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeandaa zoezi maalumu litakalowezesha kuhakiki upya vyama vya kijamii vilivyopo hapa nchini.” Alisema Nantanga.

Akifafanua Nantanga amesema pamoja na mambo mengine, zoezi hilo ambalo litaanza rasmi mwezi Oktoba 2014, linalenga kuvifuta kutoka katika daftari la Msajili vya Vyama vya Kijamii vyama ambavyo havina tena sifa ya kuendelea kuwa katika daftari hilo.

Akizungumzia sababu zinazoweza kupelekea chama kufutwa kutoka katika Daftari la Msajili wa Vyama vya Kijamii Nantanga alisema ni pamoja na kutolipa ada za mwaka kwa wakati na kutowasilisha kwa Msajili taarifa za kila mwaka za utendaji kazi wa chama.

Sababu nyingine ni chama kufanya shughuli tofauti na zile zilizoandikishwa katika katiba ya chama husika.

Ili kuvishirikisha vyama husika, Wizara wakati wa kuanza zoezi hili itachapicha katika baadhi ya magazeti majina ya vyama vyote vya kijamii vilivyopo katika kumbukumbu za daftari la Msajili wa Vyama vya Kijamii.

Baada ya kutangaza majina hayo,Nantanga alisema kila chama cha kijamii kitatakiwa kuhakikisha kuwa kinatekeleza matakwa ya kisheria ya kulipa ada ya mwaka na kuwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Kijamii taarifa kuhusu utendaji na mapato na matumizi ya fedha ya chama husika kama Sheria inavyotamka.

Baada ya kipindi cha miezi mitatu tangu kutangazwa kwa tangazo hilo, Wizara itaanza kuchukua hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kukifuta katika daftari la Msajili chama cha kijamii ambacho kitakuwa hakijatekeleza maelekezo hayo.
Pamoja na taarifa zitakazopatikana katika zoezi la uhakiki Nantanga alisema zitawezesha kuanzishwa kwa Kanzi Data ya kisasa ya vyama vya kijamii ambayo itasaidia kuboresha mawasiliano kati ya Msajili Vyama na vyama hivyo.

Aidha, baada ya kukamilika kwa zoezi hili, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itaendelea na zoezi lingine la kukagua vyama vya kijamii katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kupata taarifa zaidi kuhusu vyama hivyo.

Hadi sasa Daftari la Msajili wa Vyama vya Kijamii linaonyesha kuwepo kwa vyama vya kijamii 9,554 kote nchini,Kati ya hivyo, vyama vya kidini ni 956 na vyama vingine 8,598.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ndiyo yenye jukumu la kusajili na kusimamia uendeshaji wa Vyama vya Kijamii (Civil Societies) hapa nchini kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Kijamii SURA 337 (Societies Act Cap. 337) iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002.

Vyama vinavyosajiliwa chini ya Sheria hii ni pamoja na vyama vya kidini, vyama vya kitaaluma na vyama vya starehe na burudani.