Serikali kugharamia utafiti juu ya kinga ya Ukimwi

Baadhi ya wananchi wakiangalia viungo mbalimbali vya mwili wa binadamu ndani ya banda la Moi katika maonesho ya biashara saba saba. Kitengo cha Utafiti kutoka Moi kimefanya utafiti kupata chanjo ya Ukimwi.

Na Joachim Mushi

RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali ipo tayari kufadhili utafiti wa kinga ya Virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi (VVU), inayoendeshwa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba cha Muhimbili kwa kushirikiana na wadau kutoka ndani na nje ya nchi.

Rais Kikwete alitoa ahadi hiyo kwenye banda la Moi baada ya kupatiwa maelezo ya matokeo ya utafiti wa awali ulioendeshwa nchini na kufadhiliwa na wafadhili kutoka nje, kuangalia chanjo inayoweza kuwa kinga ya ugonjwa wa Ukimwi.

Akitoa ufafanuzi juu ya chanjo hiyo, Muuguzi Mkuu wa Kitengo cha Utafiti, Mery Ngatoluwa alisema matokeo ya utafiti walioufanya kwa kushirikiana na wadau kutoka nje na ndani, umeonesha chanjo yao iliweza kutengeneza kinga kwa asilimia 100, jambo ambalo limeleta matumaini makubwa kwenye utafiti wao.

Alisema utafiti huo uliofanyika kwa nchin za Tanzania na Msumbiji kwa awamu ya kwanza na ya pili, licha ya mafanikio ulikuwa na madhumuni ya kuangalia uongezaji wa vichocheo kwa chanjo ambavyo vingekuwa na uwezo wa kupambana na VVU ambayo ni HIVIS-03 na TaMoVac-01.

“Chanjo iliidhinishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), ili kuangalia usalama na uwezo wa chanjo katika kuongeza kinga dhidi ya VVU. Matokeo ya HIVIS-03 yalionesha asilimia 100 ya waliojaribiwa waliweza kutengeneza kinga, hata hivyo Tanzania imepata uwezo mzuri katika kuendelea na tafiti zaidi kwa wataalamu wake,” alisema.

Alisema japokuwa tafiti zaidi zitaendelea huenda zikashindikana kutokana na hali ya kutegemea fedha kutoka kwa wafadhili wan je pekee. Hata hivyo Rais Kikwete alikitaka kitengo hicho kiwasilishe ombi la ufadhili wa tafiti hizo Serikalini ili Serikali iangalie namna ya kuunga mkono jitihada hizo.