Serikali Kugawa Bure Dawa za Trakoma, Matende, Mabusha na Ngiri

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Donan Mmbando  akieleza kuhusu Mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele mbele ya Waandishi wa Habari leo 17 Desemba, 2015.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Donan Mmbando akionyesha aina ya dawa zinazotakiwa kugawiwa kwa umma wakati alipotangaza Mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele mbele ya Waandishi wa Habari leo 17 Desemba, 2015.
 
Na Shamimu Nyaki
 
SERIKALI  kupitia Mpango wa  wa Taifa wa kudhibiti Magonjwa yasiyopewa
kipaumbele imetangaza tarehe 19 hadi 23 mwezi huu kuwa itaanza zoezi la kugawa dawa kwa makundi yanayopaswa kupata dawa za magojwa hayo. 
 Tamko  hilo  limetolewa na Katibu mkuu wa Wizara Ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wazee na Watoto, Bw. Donald  Mmbando  alipokuwa anazungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kusema kuwa Magonjwa  ambayo hayapewi kipaumbele  ni Usubi, Vikope (Trakoma), Matende,
Mabusha, Ngiri maji, na Minyoo ya tumbo  hivyo dawa hizo zitasaidia kupunguza tatizo.
Ameongeza kuwa zoezi hilo la ugawaji wa dawa litatekelezwa katika vituo vyote vya Afya, Zahanati, Hospitali, shule zamsingi na sekondari, sokoni, vituo vya usafiri, pamoja na Ofisi za Serikali na Mashirika ya Umma na hivyo wananchi wanaombwa kujitokeza kwa wingi  kupata huduma hiyo ambayo haina malipo
yoyote.
Katibu Mkuu huyo  amesema kuwa wahusika wakuu katika kupatiwa dawa hizo ni Watu wote kuanzia miaka mitano na kuendelea, isipokuwa watoto chini ya miaka mitano, wajawazito, mama  anaenyonyesha mtoto chini ya siku saba na
Wagonjwa Mahututi.
“Tunataka kulinda afya zao na Uhai wao hivyo tunaomba wafuate maelekezo vizuri,” alisema Bw. Mmbando.
Aidha zoezi hilo litatekelezwa  katika mikoa ya Katavi, Rukwa, Singida,
Dodoma, Mtwara, Lindi na Pwani kwa ajili ya kujikinga  na kutibu
magonjwa hayo na Mikoa mingine iliyobaki itafanya zoezi hilo  katika  ngazi ya
jamii na shuleni mwishoni mwa mwezi Januari kuendelea hadi Februari
2016.
Naye Mratibu wa Mpango  huo Dk. Edward kirumbi ameeleza kuwa takwimu zainaonyesha kuwa magonjwa yasiyopewa kipaumbele hapa nchini ni kubwa ambapo ugonjwa wa Usubi umeenea zaidi katika mikoa sita ikiongozwa na Dodoma, Ugonjwa wa Minyoo ya tumbo wagonjwa million 13, kichocho, Matende na Mabusha tathmini za awali zinaonyesha mikoa 18  imeathirika kwa kuwa na wagonjwa million 12.
 Vile vile Dk. Kirumbi ameeleza kuwa Magonjwa haya yamekuwa na athari kubwa hasa kwa kuathiri nguvu kazi ya Taifa hivyo wananchi wanapaswa kupata dawa hizo ambazo zitakuwa zinatelewa kwa mwaka mara moja  ili kukinga upungufu wa Damu, kuuwa vimelea vya ugonjwa huo, kupungua kwa magonjwa ya ngozi, na kuongeza virutubisho bora  mwilini.
Hata hivyo jamii inapaswa kupewa
elimu zaidi kuhusu Magonjwa haya kwa vile bado haijaelewa athari za magonjwa
haya kwa  kiasi kikubwa hasa kwa maeneo
ya vijijini ambayo ndio waathirika wakubwa.