WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imepanga kufungua viwanda vya kusindika ngozi kwenye mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es Salaam ili kutoa soko kwa ngozi za wanyama wanaochinjwa kwenye machinjio ya mikoa hiyo.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Januari 18, 2016) wakati akizungumza na baadhi ya Watanzania waishio Botswana kwenye kikao kilichofanyika kwenye kituo cha mikutano ya kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana.
Waziri Mkuu alikuwa nchini Botswana kwa ziara ya siku moja kumwakilisha Rais Dk. John Pombe Magufuli kwenye mkutano wa SADC Double Troika yaani kikao maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali (SADC Summit) na Wakuu wa Nchi wanaounda Chombo cha Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ on Politics, Defense and Security Cooperation) uliofanyika kwenye kituo cha mikutano ya kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana.
Akizingumza na Watanzania hao, Waziri Mkuu alisema: “Tumeamua kufungua viwanda vya kusindika ngozi kwenye mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es Salaam (kule Pugu) ili ngozi zikishachunwa, zipelekwe moja kwa moja kiwandani,” alisema.
Alisema Serikali imeamua kuongeza viwanda nchini kama njia mojawapo ya kukuza uchumi, kuacha kuuza mali ghafi lakini pia ni fursa ya kuongeza ajira kwa Watanzania.
Akijibu hoja zilizoainishwa kwenye risala yao, Waziri Mkuu alisema Serikali bado ina nia ya kuhamia Dodoma na kwamba itaendelea kutenga fedha zaidi ili wizara nyingi zijenge ofisi zao Dodoma. “Serikali ilikwishaamua kwamba Dodoma ni mji wa kiserikali na Dar es Salaam ni mji wa kibiashara. Kwa sasa kuna baadhi ya Wizara zimeshajenga ofisi Dodoma na kuna taasisi kama vile Benki Kuu nazo pia zimejenga ofisi zake Dodoma. Tutaendelea kutenga fedha zaidi ili wizara nyingine zikamilishe ujenzi wa ofisi zao,” alisema.
Waziri Mkuu Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora) watafute fedha za mitaji ama zao ama kupitia kwa marafiki zao ili waweze kuwekeza nyumbani (Tanzania).
“Nia ya Serikali sasa hivi ni kufungua milango kwa wawekezaji hasa wenye nia ya kujenga viwanda. Njooni nyumbani muone ni eneo gani mnaweza kuwekeza, kama mna miradi huku fungueni matawi kule nyumbani. Serikali inajivunia uwepo wenu kwa sababu inatambua kwamba huku mliko kuna kitu mnajifunza na mnaweza kukirudisha nyumbani kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla,” alisema.
Mapema, akisoma risala yao kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Chama cha Watanzania waishio nchini Botswana (The Association of Tanzanians in Botswana – ATB), Bw. Neiman Kissasi alisema chama hicho kilianzishwa mwaka 1992 kikiwa na lengo la kuwaunganisha Watanzania waishio Botswana pamoja kujenga undugu wao na kusaidiana.
Katika risala yao, walishauri wafugaji wa Tanzania waelimishwe na kuwezeshwa kufuga kisasa na kuondokana na ufugaji wa kurandaranda. Pia waliiomba Serikali iongeze kasi ya mpango wake wa kuhamisha shughuli zote za Serikali mjini Dodoma, kwani itasaidia kupunguza matumizi ya Serikali kwa kuwa shughuli za Serikali zitakuwa zinafanyika eneo moja.
Vilevile, waliiomba Serikali ifungue fursa za kiuchumi kwenye mikoa mingine ya Tanga, Lindi, Mtwara, Pwani, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Arusha badala ya kuziacha ziwe Dar es Salaam peke yake. “Hii itasaidia kuibua fursa za kiuchumi na kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam”, ilisema sehemu ya risala yao.
Waziri Mkuu alirejea jijini Dar es Salaam jana usiku (Jumatatu, Januari 18, 2016.)