Serikali kufufua kilimo cha kahawa


Na Immaculate Makilika- Maelezo
 SERIKALI imeandaa mkakati wa kuendeleza  kilimo cha kahawa ( Tanzania Coffee Industry Development  Strategy,2012-2022) kwa lengo la kuendeleza kilimo cha  zao  hilo  nchini kupitia Bodi ya kahawa  nchini  na kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo.
Aidha  Serikali imefafanua  kuwa hatua hiyo ni  kuongeza uzalishaji ,tija na ubora wa kahawa Kitaifa ili kuboresha mapato ya wakulima wa zao hilo  katika mikoa mbalimbali inayolilima  ikiwemo mkoa wa Kilimanjaro .
Kauli hiyo ilitolewa leo Bungeni na Waziri wa  Nchi Ofisi ya Mahusiano  na  Uratibu  Steven Wassira kwa niaba  Waziri wa Kilimo ,Chakula na Ushirika , Chrisopher Chiza , wakati akijibu swali la  Grace   Kiwelu(Mbunge Viti Maalum-CHADEMA) aliyeuliza  Je,Serikali ina mpango gani  madhubuti na mahsusi wa kufufua kilimo cha Kahawa mkoani Kilimanjaro  ambacho  kwa miaka mingi kimekua tegemeo kwa wananchi  wa Kilimanjaro na mhimili mkubwa kwa uchumi wetu wa Taifa letu.
 Alisema malengo mahsusi ya mkakati huo ni pamoj ana kuongeza na uzalishaji  wa kahawa safi kutoka wastani wa sasa wa tani 50,000 kwa  mwaka hadi kufikia tani  100,000 ifikapo mwaka 2022 na kuongeza ubora  wake  ili kupata bei ya ziada katika masoko ya nje kutoka wastani wa asilimia  35 hadi kufikia wastani wa asilimia 70 ifikapo  mwaka 2022.
Aidha Wassira alisema maeneo muhimu katika mkakati huo ni pamoja na kuimarisha huduma za ugavi  ili wakulima wazingatie kanuni bora za kilimo,kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI) ili kuhakikisha  upatikanaji wa miche bora ya kahawa ,pamoja  na kuongeza matumizi ya viwanda vya kati vya kuitayarisha  ili kuongeza ubora wa zao hilo na hivyo wakulima kunufaika na bei nzuri.