Na Eleuteri Mangi
UZEE na kuzeeka ni dhana inayoelezea hatua ya mwisho ya makuzi ya binadamu kuanzia utoto, ujana hadi kufika hatua ya mwisho ya makuzi ambayo ni uzee. Binadamu ni miongoni mwa viumbe hai ambao hupitia hatua hizo katika makuzi yake, mwanasikolojia Erick Erickson aliyeishi kati ya miaka ya 1902-1994 amebaisha kuwa binadamu hupita hatua nane za makuzi hayo ikiwemo hatua ya uzee. Kulingana na Erickson, Uzee ni hatua ya nane na ya mwisho katika maisha ya mwanadamu, hatua ambayo umri wake unaanzia na miaka 65 na kuendelea amabapo hutawaliwa kwa hekima, busara na kupungukiwa na nguvu za kufanya kazi ngumu kupita uwezo wao.
Katika nchi zilizoendelea kama Uingereza na Marekani, suala la uzee linahusishwa na umri wa kustaafu ambao ni miaka 65. Katika nchi nyingine umri wa kustaafu unatofautiana kijinsi, kwa mfano, nchini Latvia wanaume wanastaafu wakiwa na miaka 55 wakati wanawake wanastaafu wakiwa na umri wa miaka 60. Hapa Tanzania mtu anaitwa mzee kutokana na ama umri mkubwa, majukumu aliyonayo na pia hadhi yake, kwa mfano mkuu mahali pa kazi au katika ukoo.
Mwandishi wa makala haya anatumia dhana ya wazee tulionao katika nchi yetu kuwa aidha walikuwa wanafanya kazi za kuajiriwa au kujiajiri au ni wale walioko vijijini ambao kuzeeka kwao ni matokeo ya kupungukiwa nguvu za kufanya kazi.
Tanzania pamoja na ukweli kwamba watumishi walio katika Serikali na Taasisi zake wanastaafu wanapofikia miaka 60 na kwamba wazee wa vijijini na wale waliojiajiri wanakoma kufanya kazi kutokana na kuishiwa nguvu, ukweli unabaki kwamba binadamu mwenye umri wa miaka 60 anaonyesha dalili za hatua hiyo. Kama mataifa ya dunia hii, Tanzania inajali na kutambua umuhimu wa wazee ikiamini kuwa wao ni kisima cha hekima na busara katika Maisha ya kijamii na taifa.
Ni ukweli usiopingika kuwa “wazee ni hazina”, jambo ambalo linatuaminisha palipo na wazee haliharibiki jambo kwani wao ni rasilimali na ni hazina kubwa ya maendeleo. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutambua umuhimu wa wazee amekuwa na desturi ya kuwatumia mara kwa mara katika kutekeleza majukumu yake kitaifa na kimataifa.
Rais Kikwete anamini juu ya usemi wa “wazee ni hazina” na amekuwa akiongea nao kila anapoona ni muda muafaka kufanya hivyo. Ipo mifano hai ya Rais Kikwete alipozungumza na wazee hao ikiwemo Mei 03, 2010 aliongea na wazee wa mkoa wa Dar es salaam juu ya mkutano wa kimataifa kuhusu masuala ya uchumi uliofanyika nchini Mei 05 hadi 07, 2010.
Mwaka huo huo aliongea na wazee wa Dar es salaam mnamo Julai 30, 2010 ambapo mara hii Rais Kikwete alikutana Ikulu na wazee wakongwe wa kivita nchini na wanachama wa Tanzania Legion and Club kuhusu masuala yao ikikumbukwa kuwa wazee hawa walilitumikia taifa lao kwa umahiri mkubwa. Wazee hawa vili vile ni washauri wakuu na walinda amani. Hali hii inadhihirika kunapotokea migogoro mabilimbali katika jamii nyingi ambapo wazee hutumika kama hatua za awaali katika kusuluhisha na hatimaye kupata ufumbuzi wa migogoro hiyo.
Kwa kuwajali, kuwalinda na kuwathamini, Umoja wa Mataifa umetenga siku ya tarehe Oktoba Mosi ya kila mwaka kuwa ni Siku ya Wazee Duniani. Siku hii imetengwa kufuatia uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Wazee katika azimio Na.46 la mwaka 1991. Nafasi hii imetengwa ili kuyawezesha mataifa kutafakari nafasi ya wazee katika jamii kwa kuzingatia mahitaji, matatizo na ushiriki wao katika maisha ya kila siku.
Tanzania ambayo ni nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, imekuwa ikiadhimisha siku hii kitaifa kila mwaka ambapo mwaka huu ilifanyikia wilaya ya Korogwe mkoani Tanga. Kwa kawaida siku ya Wazee Duniani huadhimishwa kwa kuzingatia ujumbe maalumu wa mwaka ambao ni dira na kichicheo chenye dhana ya uhamasishaji kwa wananchi. Lengo kubwa ni kuwawezesha kupata ufahamu na hatimaye kuweka mikakati ya utekelezaji wa masuala muhimu yaliyoamuliwa Kitaifa na Kimataifa.
Maadhimisho ya mwaka jana yaliongozwa na kauli mbiu iliyotafsiriwa na wazee wenyewe iliyosema “Matarajio ya Wazee ni Heshima, Usalama na Maisha Bora” tafsiri waliyoitoa kutoka kauli mbiu iliyotolewa na Umoja wa Mataifa “The future we want: what elder persons are saying”.
Kama taifa hatunabudi kujikumbusha na kutafakari maneno ya busara yaliyotamkwa na aliyekuwa Kaibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Koffi Anan, “Huwezi kufurahia usalama bila maendeleo, hatuwezi kufurahia maendeleo bila usalama na hatuwezi kufurahia hivyo vyote bila kuheshimu haki za binadamu” Katika kuadhimisha siku ya Wazee Duniani, kuna mambo ambayo Tanzania kama taifa imefanya juhudi na itaendelea kufanyia kazi kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyojieleza.
Nchi yetu imekuwa ikizingatia misingi ya sheria na utawala bora na hivyo kudumisha amani, heshima na kujali maisha ya watu wake. Katika kuadhimisha siku ya Wazee Duniani mwaka huu, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal, alisema kuwa nia ya Serikali ya kupambana na vitendo vya uvunjifu wa amani katika nchi yetu bado ipo palepale.
Dk. Bilal alisisitiza, “Nawasihi Watanzania wote tushirikiane bega kwa bega na Serikali katika kujenga, kulinda na kudumisha amani kwa wazee”. Katika kuadhimisha Mwaka wa Kimataifa wa Wazee (1999) Serikali ilifanya maamuzi ya kuwa na Sera ya Taifa ya Wazee. Maamuzi ya kuwa na Sera hii ni kielelezo cha dhamira hai na dhati ya Serikali ya kuweka masuala ya wazee katika agenda ya maendeleo ya nchi yetu.
Serikali inatambua kwamba wazee wetu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na umaskini, kutotosheleza kwa huduma za afya, pensheni na kutoshirikishwa katika maamuzi muhimu yanayohusu maendeleo ya nchi yao. Pamoja na hali hii, Serikali inatambua kwamba wazee ni raslimali na nguvu mpya katika maendeleo ya nchi. Jitihada zitaendelea kuwekwa kuhakikisha kwamba wazee wanatambuliwa na wanapata fursa ya kushiriki katika shughuli za maendeleo ya nchi yao sanjari na wananchi wengine.
Kuwapo kwa Sera ya Taifa ya Wazee ni hatua ngeni kwa nchi nyingi, Tanzania ikiwa moja wapo. Katika bara la Afrika, Tanzania imekuwa nchi ya pili kuwa na Sera ya aina hii baada ya Mauritius. Endapo kutatokea upungufu katika matamko na utekelezaji wa Sera yenyewe Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii itakuwa tayari kufanya marekebisho pale yanapohitajika.
Kwa Serikali, watumishi wa umma na jamii nzima, Sera ya wazee kwa taifa letu ni mwongozo katika kuandaa mipango, utekelezaji na tathmini utoaji huduma kwa wazee. Hivyo, Serikali itaendelea kuwaenzi wazee wetu kwa heshima, usalama na maisha bora suala ambalo ni msingi na nguzo kwa maendeleo yetu. Maisha bora yatakuja kama tutawawezesha makundi maalumu katika jamii wakiwemo wazee.
Kwa kupitia takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa kuhusu sense ya watu na makazi iliyofanyika Agosti 26, 2012 zinaonesha kuwa kuna jumla ya wazee Tanzania ni 2,507,568 sawa na asilimia 5.6 ya Watanzania wote. Jumla hii inaundwa na wazee wanakiume 1,200,210 sawa na asilimia 5.5 na wanakike 1, 307, 358 sawa na asilimia 5.7.
Tofauti na sense ya watu na makazi ya mwaka 2002 ambapo wazee wazee walikuwa asilimia 4.0, Tasira hii inaonesha kuwa idadi ya wazee nchini imeongezeka kwa tofauti ya asilimia 1.6, tofauti hii inaonesha taswira na mwelekeo kuwa kuwa idadi ya wazee chini wataendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka. Itakumbukwa kuwa tangu mwaka 2002, Tanzania ilipoungana na mataifa mengine duniani kutia saini ya Mkataba wa Kimataifa wa wazee ilikuwa ni kielelezo tosha cha kuwathamini wazee na hivyo kuanza kubuni, kuweka mipango mbalimbali yenye lengo la kuboresha maisha yao.
Katika maadhimisho siku ya Wazee Duniani mwaka huu, Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Seif S. Rashid, ametaja kuwa baadhi ya mipango ambayo Serikali imetekeleza ni pamoja na kuwepo kwa Sera ya Taifa ya Wazee iliyotungwa 2003 kwa ajili ya kusimamia mipango na mikakati mbalimbali inayolenga wazee na hivyo kutambuliwa kwao kama kundi pekee na ushiriki wao katika mipango ya maendeleo ya taifa.
Naibu Waziri Rashid alikiri na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za hari, hii ni katika hatua ya kuboresha huduma zitolewazo katika makazi 41 yanayowatunza wazee wenye shida na wasiona ndugu wa kuwatunza hapa nchini.
Akitoa msimamo wa Serikali Naibu Waziri alisema, “Thamani ya mchango wa wazee inatambuliwa na Serikali hasa inapoendelea kuboresha utaratibu wa utoaji matibabu kwa wazee wote bila malipo”.
Eneo hili linaendelea kuboreshwa ili huduma kwa wazee zitolewe bila vikwazo vyovyote. Kwa kuzingatia Waraka wa Serikali uliotolewa Februari mosi, 2007, Serikali imetoa msamaha wa kodi ya majengo wanayoishi wazee na yasiyokuwa ya biashara.
Ili kulinda usalama wa wazee, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo imeendelea kuchukuahatua kali za kisheria kwa wale wote wanaobainika kujihusisha na mauaji ya wazee.
Vile vile, Serikali itaendelea kuelimisha jamii juu ya madhara yatokanayo na vitendo viovu dhidi ya wazee. Kwa kutambua mchango mkubwa na umuhimu wa wazee, Serikali imewashirikisha wazee katika kutoa maoni yao katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu masuala yao. Katika kuwaenzi wazee, ni dhahiri kama taifa litaendelea kunufaika na michango yao, hivyo hatuna budi kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuishi ili waendelee kuchangia katika maendeleo ya taifa. Kuwepo kwa taifa lenye amani ni matokeo ya misingi mizuri walioijenga wazee wetu tangu hapo awali kwa kuwajali, kuwaenzi watu wote bila kujali umri na hali zao za maisha katika hatua mbalimbali kama zilivyoainishwa na Mwanasikolojia Erick Erickson.