Serikali Kuendelea Kujenga Barabara kwa Kiwango cha Lami

Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano   Eng Godwin Ngonyani akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha Bunge la 11 linaloendelea Mjini Dodoma. picha na Raymond Mushumbusi MAELEZO

Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Eng Godwin Ngonyani akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha Bunge la 11 linaloendelea Mjini Dodoma. picha na Raymond Mushumbusi MAELEZO

Na Raymond Mushumbusi MAELEZO

Serikali imeahidi kuendelea na ujenzi wa barabara katika maeneo tofauti nchini kwa kiwango cha lami ili kutatua adha kubwa ya ubovu wa barabara ulipo katika maeneo mengi nchini.

Hayo yamesemwa leo Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Eng Godwin Ngonyani akijibu maswali ya wabunge waliouliza kuhusu mpango wa serikali kuboresha barabara zilizopo na kujenga mpya ili kukabiliana na adha ya ubovu wa barabara nchini.

Akijibu swali la Mhe Richard Mganga Ndassa Mbunge wa Sumve (CCM) lililohitaji ufafanuzi wa serikali ni lini ujenzi wa barabara ya Magu-Bukwimba –Ngudu-Hungumalwa itajengwa kwa kiwango cha lami, Mhe Eng Godwin Ngonyani amesema katika mwaka wa fedha 2014/15 na 2015/16 serikali ilitenga jumla ya shilling millioni 200 kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 70 na taratibu za kumtafuta Mhandisi Mshauri zinaendelea na baada ya kukamilika kwa usanifu na kupata gharama za mradi huo, Serikali itatafuta fedha za kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Aidha akijibu pia swali la Mhe Fredy Atupele Mwakibete Mbunge wa Busokelo (CCM) aliyehitaji kujua ni lini barabara ya Katumba-Mbambo-Tukuyu yenye urefu wa Kilometa 82 inayoanzia Katumba(RDC) kupitia Mpombo,Kandete,Isange,Lwanga, Mbambo (BDC) hadi Tukuyu (RDC) itajengwa kwa kiwango cha lami.

Akijibu swali hilo, Mhe. Eng Godwin Ngonyani amesema kuwa Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, katika mwaka wa fedha 2009//10 Serikali ilianza maandalizi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami na ambapo upembuzi yakinifu na sanifu wa kina ulikamilika na baadae Serikali iliamua kujenga kilometa 10 ambapo mwezi April,2014 Wakala wa Barabara na kampuni ya CICO ilijenga barabara hiyo kuanzia Lupaso hadi Buseji,Wilayani Busokelo.

Serikali kupiti Wakala wa Barabara (TANROADS) inaendelea na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika Kata, Wilaya na Mikoa mbalimbali nchini ili kukabiliana na adha ya ubovu wa barabara ambao umesababisha watu kukosa mawasiliano baina ya maeneo.