SERIKALI KUANGALIA UPYA GHARAMA ZA BEI YA MAFUTA

Wananchi wakiwa kwenye foleni kununua mafuta ya petroli

Na Veronica Kazimoto – MAELEZO, Dodoma

21/6/2011,

SERIKALI inaandaa utaratibu wa kupitia upya mchanganuo wa tozo zilizopo katika nishati ya mafuta kwa lengo la kupunguza makali ya maisha na bei ya nishati hiyo inayosababisha mfumko wa bei ya bidha mbalimbali nchini.
Akijibu swali la Mbunge wa Handeni Dk. Abdallah Kigoda leo mjini Dodoma kuhusu athari za mfumuko wa bei kwa wananchi wa kipato cha chini Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi Pereira Ame Silima amesema hatua hiyo inafuatia athari za mfumuko wa bei ya bidhaa mbalimbali iliyosababishwa na kupanda kwa gharama za bei ya mafuta nchini.
Amesema Serikali kwa kuliona hilo imeanza kuchukua hatua ya kuuza kwa wananchi sehemu ya chakula kutoka katika hazina ya nafaka ya taifa kwa bei ya chini ili kuwawezesha wananchi kununua chakula kwa bei nafuu.
“Hivi sasa serikali imeanza kuuza sehemu ya chakula kutoka katika hazina ya nafaka ya Taifa kwa bei ya chini ili kuhakikisha kuwa wananchi wenye vipato vya chini wanamudu kununua nafaka hizo,”
Aidha ameyataja maeneo mbalimbali ya kimkakati yatakayoweza kupunguza athari za mfuko wa bei nchini kuwa ni pamoja na usimamizi wa karibu wa ujazo wa fedha kwenye uchumi, uongezaji wa uzalishaji wa nishati kwa kutumia vyanzo mbalimbali vilivyopo nchini kama gesi, upepo, jua na makaa ya mawe.
Maeneo mengine ni ukamilishaji wa taratibu za ununuzi wa mafuta kwa wingi, kuongeza upatikanaji wa chakula kwa kuhimiza kilimo cha umwagiliaji pamoja na kuimarisha miundobinu ya barabara ili kupunguza gharama za usafirishaji wa mazao ya kilimo na bidhaa kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Hata hivyo Mh. Pereira ametoa wito kwa wananchi kuendelea kulima mazao yanayohimili ukame, kutilia mkazo kilimo cha umwagiliaji na kujiwekea akiba ya chakula cha kutosha kutokana na mahitaji ya kaya na kuzihimiza sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika uwekezaji kwenye kilimo na nishati ili kusaidia kupunguza makali ya gharama za maisha kwa wananchi wa kipato cha chini na kukuza uchumi kwa ujumla.