Kule Kasulu mkoani Kigoma, wiki hii limeripotiwa tukio la kutisha kwamba Jeshi la Polisi linawashikilia askari wake wanane wa kituo chake wilayani humo kwa tuhuma za kumtesa, kumpa kipigo na kumuua raia, Festo Andrea akituhumiwa ujambazi wa kutumia silaha.
Ikadaiwa kuwa askari hao walimpiga kichwani na kwenye mbavu kwa kutumia kitako cha bunduki na kumwekea miti kwenye sehemu zake za haja kubwa.
Tukio hili lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai kwamba lilitokea Kasulu Agosti 8 mwaka huu majira ya saa 8 mchana.
Mkuu wa wilaya ya Kibondo anayekaimu nafasi ya Mkuu wa wilaya ya Kasulu, Danny Makanga aliyeunda kamati kuchunguza tukio hilo alieleza baada ya uchunguzi kwamba ni kweli polisi hawa walihusika na kumpiga Festo na kumsababishia kifo.
Ripoti ya daktari nayo ilithibitisha kifo cha Festo kilitokana na kipigo kilichosababishwa na kupasuka kwa bandama. Ushahidi mwingine ulitoka kwa viongozi wa kata akiwemo diwani.
Kusema ukweli tukio hili linasikitisha sana hasa ikizingatiwa kwamba wanaodaiwa kusababisha kifo cha kijana huyo ni polisi waliokula kiapo cha utii kuzingatia maadili na kutekeleza sheria katika utendaji wao.
Na kikubwa zaidi, polisi wetu wakati wanakula kiapo, huapa kulinda raia na mali zao. Pamoja na ukweli huo, inasikitisha kuona baadhi wanatenda kinyume badala ya kulinda raia wanashiriki katika kuwasababishia madhara ikiwa ni pamoja na kifo.
Swali ni je, kama kweli kijana huyo alikuwa na tuhuma zinazomkabili, baada ya kufuatwa nyumbani na kupelekwa kwa mtendaji, kisha kuchukuliwa na polisi, kwanini hakufunguliwa mashtaka ili sheria itende haki?
Kwanini polisi hawa walichukua sheria mkononi na kuanza kumpiga kijana yule na kumfanyia mateso yote hayo pamoja na ndugu yake aliyefika kutaka kujua kosa la nduguye na akaunganishwa naye kwa uonevu?
Mateso kwamba walipigwa kwa vitako vya bunduki, kuwaingiza vijiti sehemu ya haja kubwa, chupa za bia, tena hadharani mbele ya baba yao mzazi na kulazwa ndani ya gari kifudifudi kisha kuwekewa magunia ya mkaa migongoni ilikuwa ni ukatili mbaya sana.
Hawa ndio polisi wetu ambao raia wanaambiwa kila wakati kuwa ni walinzi wao wa amani na hivyo kila litokeapo jambo la kihalifu watoe ushirikiano ili kuleta amani na utulivu. Kama wanatesa raia kiasi hiki bila ushahidi wa tuhuma, wamuegemee nani?
Serikali yetu pamoja na Jeshi letu la Polisi yafaa lizinduke na kukabili matukio haya ambapo baadhi ya polisi wanaolichafua jeshi na serikali, na hivyo kupoteza imani ya wananchi juu yake. Matukio haya yanaharibu sura na sifa nzuri ya jeshi letu na serikali yetu kwa jumla, hivyo yakomeshwe.
Tukio kama hili mazingira yote yanaonyesha kuwa polisi hao walihusika katika kusababisha kifo cha raia huyo. Ili wananchi warejeshe imani thabiti, hatua madhubuti lazima zichukuliwe dhidi ya wahusika wote.
IGP Mwema tunamuomba akae tena na polisi wetu kuwakumbusha majukumu yao. Kazi yao siyo kuua raia, kama ni mtuhumiwa na amekamatwa afikishwe kwenye sheria badala ya kumdhuru mtu asiye na silaha wala uwezo wa kupambana nao.
Na endapo itathibitika kuwa askari hao wamehushika kifo cha kijana huyo, hatua kali zichukuliwe dhidi yao. Uonevu huu ni hatari kwani unajenga chuki mbaya kati ya raia na polisi, hivyo ni muhimu sana ukomeshwe na kupigiwa kelele hasa wakati huu taifa linaadhimisha miaka 50 ya Uhuru wetu.