Na Joachim Mushi
KITUO cha Habari Kuhusu Ulemavu (ICD) kimeiomba Serikali kuanza utekelezaji wa makubaliano ya mkataba wa watu wenye ulemavu ulioridhiwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (AU), tangu mwezi Mei mwaka jana.
Asasi hiyo mwanaharakati kwa wenye ulemavu imesema inapatwa na hofu kuamini kwamba Serikali ina nia ya dhati ya kutekeleza mkataba huo wa watu wenye ulemavu, kutokana na ukimya wake wa kuanza kwa utekelezaji hadi sasa.
Changamoto hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam ndani ya banda la Maonesho ya 35 ya Biashara Kimataifa la ICD na Ofisa Habari wake, Mohamed Kajembe alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari kuelezea masuala mbalimbali ya utendaji wa asasi.
Kajembe alisema ICD pamoja na wanaharakati wengine wa haki za binadamu hasa kwa walemavu wamekuwa wakishangazwa na kitendo cha Serikali, kuanza kutekeleza makubaliano ya haki za watu wenye ulemavu ambayo iliridhia tangu Mai, 2010.
Alisema ili kutoa wigo mpana kwa watu wote kuuelewa mkataba huo, ICD imeutafsiri kwa lugha ya Kiswahili makubaliano hayo na kutoa nakala kwa AU na kuuweka mkataba huo kwenye maktaba yao kwa ajili ya wananchi wa kawaida kuupitia na kuelewa kilichoridhiwa ndani.
Aidha Ofisa Mradi wa kituo hicho, Anania Abel ameitaka Serikali kuhakikisha inaingiza makubaliano ya mkataba wa haki za wenye ulemavu katika mchakato wa uundaji katiba mpya unaoendelea, ili masuala muhimu ya haki za jamii hiyo yaingie kwenye Katiba mpya ya nchi inayotarajiwa kuundwa.
Aliongeza kuwa kwa sasa kuna haja ya Serikali kuingiza haki za walemavu katika utekelezaji wa sera na sheria ili jamii hiyo iweze kuzidai kisheria na hata kulalamika kwenye vyombo vinavyo tafsiri sheria pale wanapoona hakuna utekelezaji uliofanywa.
“Unajua bado mambo mengi juu ya utekelezaji wa masuala ya haki za walemavu yapo kihisani…yaani mamlaka husika zinafanya kama kutoa msaada kwa kundi hili. Hii sisi tunaona haifai inatakiwa ijengwe miundombinu ya kuweza hata kuishtaki pale wanapokwenda kinyume na makubaliano,” alisema Abel.