TUNASIKITISHWA na namna ambavyo serikali imekuwa ikishughulikia suala laupungufu wa dawa na vifaa tiba nchini. Siku za karibuni, kumekuwepo na taarifa za ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika sehemu mbalimbali nchinilakini serikali bado haijachukua hatua madhubuti, jambo ambalo linaweza kuchangia wagonjwa kuteseka zaidi na hata kusababisha vifo.
Sikika ilitegemea serikali ingeangalia janga hili kwa makini zaidi na kulipa mara moja deni lote (Tshs bilioni 90), linalodaiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Badala yake ni Tshs. bilioni 20 tu zilizotolewa mpaka sasa na nyingine Tsh bilioni 11 zilizoahidiwa kutolewa ndani ya mwezi mmoja. Kutokana na unyeti wa suala hili ambalo linagusa maisha ya wananchi, tungependa kuona serikali ikilipa fedha zote inayodaiwa na MSD ili kuiwezesha kufanya kazi ipasavyo na kupunguza upungufu wa dawa na vifaa tiba uliojitokeza nchini.
Deni la MSD lilitakiwa kulipwa tangu kitambo na mikakati ya kuzuia ongezekola deni hilo ilitakiwa iwepo na itekelezwe. Mara nyingi na kwa nyakati tofauti tofauti wabunge, hususani Kamati ya Kudumu ya Huduma za Jamii wamekuwa wakiitaka Serikali kuilipa MSD deni linalodaiwa.Tunaamini kwamba hali iliyopo sasa ingeweza kuzuilika kama Serikali ingesikiliza na kufanyia kazi maagizo ya Bunge kwa wakati. Badala yake, deni limekuwa likiongezeka huku mikakati ya kulipa deni hilo ikiwa haina tija.
Tatizo la uhaba wa dawa na vifaa tiba linaloendelea kwa sasa linasababishwa na kukua kwa deni na hivyo kuifanya MSD kushindwa kusambaza dawa na vifaa tiba kwa vituo vya kutolea huduma vyenye madeni. Hata hivyo, tatizo la upungufu wa dawa na vifaa tiba nchini ni sugu na linapaswa kutatuliwa. Sababu kuu zinazosababisha uhaba wa dawa nchini ni bajeti ndogo inayotengwa, ucheleweshaji katika kutoa fedha zilizotengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa pamoja na takwimu zisizo sahihi juu ya mahitaji halisi ya dawa nchini. Hivyo, ni vyema Serikali ikatatua pia vyanzo vingine vinavyosababisha uhaba wa dawa nchini pamoja na kulipa deni kamili.
Kwa mfano, katika hospitali ya Sinza Palestina, walikuwa wakidaiwa na MSD Tsh. milioni 93. Oktoba mwaka huu, walipokea fedha kutoka Mfuko wa Afya wa pamoja (health basket fund) na kuagiza MSD dawa na vifaa tiba vyenye gharama ya Tsh. milioni 100. Hata hivyo, walipokea mzigo wenye thamani ya Tsh. milioni 25 tu kwa sababu MSD walikata deni wanalowadai la Tsh. milioni 75.
Hii imelazimisha hospitali hiyo kutumia dawa walizopokea kwa ajili ya dharura tu, kwa sababu dawa hizo haziwezi kukidhi mahitaji yao ambapo wanahudumia takribani wagonjwa 600 kwa siku, hivyo kusababisha uhaba wa dawa katika hospitali hiyo, kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa na vyombo vya habari. Hali hii katika hospitali ya Sinza Palestina inafanana na hospitali nyingi nchini. Ni wakati muafaka sasa wa Serikali kuhakikisha tatizo la uhaba wa dawa na vifaa tiba nchinilinakwisha na kubaki kuwa historia.
Sikika inatoa wito kwa Serikali kufanya jitihada za makusudi katika kumaliza tatizo hili sugu la uhaba wa dawa katika vituo vya huduma za afya kwa kushughulikia mzizi wa tatizo na si kusubiri kutatua matatizo yanayoibuka mara kwa mara. Hivyo basi, Sikika inashauri bajeti ya dawa iongezwe kufikia angalau nusu ya mahitaji ya nchi, ambayo ni Tsh. bilioni 250 kwa mwaka. Pia tunashauri kuwa Wizara ya Fedha na Uchumi (MoFEA)kutoa gawio la fedha zote zinazotengwa kwa ajili ya dawa na vifaa tiba kwa mkupuo mmoja kwenda kwenye akaunti za vituo MSD. Gawio hilo litolewe mwanzo wa mwaka ili kuiwezesha MSD kununua dawa hizo kwa wakati.
Pia tunaitaka MSD kuimarisha mfumo mzima wa ununuzi na usambazaji wa dawa na vifaa tiba nchini kwa kuhakikisha kuwa hakuna upungufu katika maghala yao. Ni vema MSD ikaondokana na kuchelewa kwa usambazaji wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma na kuimarisha mfumo wa kufidia pale ambapo dawa zimekosekana au kutolewa katika idadi ndogo. Mwisho, MSDiboreshe utendaji wa kazi, uwazi na uwajibikaji kwa sababu hizo ndizo nguzo borakatika mfumo wa ununuzi na usambazaji wa dawa .
Sikika ingependa pia kuelimisha tena umma kuwa kusitishwa kwa misaada ya fedha na wahisani ni kwenye bajeti ya maendeleo tu na sio kwenye mfuko wa pamoja wa afya (Health Basketi Fund) kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa na baadhi ya watu. Mfuko wa pamoja wa afya unaotolewa na wahisani kwenye halmashauri, theluthi ya fedha hizo zinapaswa kutumika katika ununuzi ya dawa muhimu na vifaa tiba.
Mwisho, Sikika inapenda kuwapongeza Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dr. Seif Rashid na Katibu Mkuu wake Dr. Donan Mmbando kwa kutoa tamko la kusitisha kutumika kwa viwango vipya vya gharama za matibabu katika hospitali ya taifa ya Muhimbili. Gharama hizi mpya si kwamba zingewanyiwa wananchi walio wengi haki ya kupata huduma bora za afya bali pia si sahihi kuwalipisha zaidi wagonjwa ili kulipa deni ambalo hawakuhusika nalo.
Mr. Irenei Kiria,
Executive Director of Sikika,