Na Magreth Kinabo, Maelezo
MSEMAJI wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene amesema Jaji Joseph Warioba alitunukiwa tuzo ya muungano iliyotukuka kwa kuwa alistahili, kama viongozi wengine na si kweli kwamba kitendo hicho ilikuwa kumkejeli kama baadhi ya vyombo vya habari vilivyoripoti hivi karibuni. Hayo yalisemwa leo na Mkurugenzi Mwambene wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na suala hilo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ukumbi wa Idara ya Maelezo jijini Dar es Salaam.
“Kumekuwa kuna taarifa katika baadhi ya magazeti kuwa Serikali kumpa tuzo Jaji Warioba ni kumkejeli, Ninapenda kuwataarifu kuwa kitendo cha Serikali kumpa tuzo Jaji Warioba haikumkejeli wala kumtukana. Jaji Warioba anastahili kupewa tuzo kama mawaziri wakuu wengine kwa kuwa mchango wake katika muungano unajulikana,” alisema Mwambene.
Tuzo hiyo aliyoipewa Jaji Warioba, wakati wa maadhimisho ya mika 50 ya Muungano wa Tangayika na Zanzibar. Mwambene aliongeza kuwa tuzo hiyo haihusiani na mjadala wa Rasimu ya Katiba. Alifafanua kuwa katika mjadala wa Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba uliokuwa ukifanyika katika Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma, baadhi ya wajumbe walikuwa wanatoa mawazo yao na si kwamba wanapingana na Jaji Warioba
“Mjumbe anatoa mawazo yake wakati wa kujadili kwa kuwa hiyo bado ni rasimu, hivyo hapingani na Jaji Warioba,” alisisitiza huku akisema rasimu huwa inafanyiwa marekebisho.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo, alisema bado Ofisi yake inaendelea na hatua ya pili kuhusu gazeti la MAWIO kutoa maelezo ya kuchapisha habari yenye kichwa cha habari ‘Hati Muungano Utata’. Mwambene alifafanua kuwa ofisi hiyo inaendelea na suala hilo kwa hatua hiyo ili kutoa nafasi kwa viongozi husika wa gazeti kutoa maelezo baada ya hapo awali kupeleka barua ya kutaka maelezo hayo kwenye ofisi za gazeti la ‘MAWIO’ na kukuta zimefungwa.
Aidha alisema kuwa hata majirani wa ofisi hizo walikataa kupokea barua hiyo, kwa maelezo kuwa kama ni masuala ya habari wahusika ndio wanapaswa kuipokea. Aliongeza kwamba ofisi yake itafanya maamuzi sahihi ikiwahaitapata maelezo hayo, hivyo isijeikalaumiwa. Mwambene aliwataka waandishi wa habari kuwa na kitambulisho cha uandishi wa habari (Press Card) na ametoa muda wa wiki moja kuanzia leo kwa mwandishi ambaye hana ili kuweza kukamilisha taratibu za kukipata.
Pia amewataka waandishi wa habari kuwa na heshima katika utendaji kazi wa taaluma hiyo na kuzingatia mavazi yanayostahili kwani wao ni kioo cha jamii.