WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Prof. Makame Mbarawa amemtaka mkandarasi anayejenga barabara ya Mwenge – Moroco KM 4, kuhakikisha inajengwa kwa ubora uliokusudiwa na kukamilika kwa wakati ili kumaliza adha ya msongamano wa magari katika eneo hilo. Akikagua ujenzi wa barabara hiyo Prof. Mbarawa amemtaka Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dar es salaam kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na hatua kali zinachukuliwa kwa watu wote watakaozembea na kuhujumu miradi ya barabara.
“Kipaumbele chenu kiwe ubora na kufanya kazi kwa haraka ili barabara hii ikamilike katika wakati uliopangwa na hivyo kuondoa usumbufu kwa wananchi,” amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Akizungumza na wafanyakazi wa TANROADS makao makuu Prof. Mbarawa amesema serikali haitawavumilia watumishi wazembe wanaofanya kazi chini ya kiwango au kwa uzembe. Amewataka TANROADS kuhakikisha hakuna misururu mirefu katika vituo vya mizani zote nchini na kupambana na rushwa katika ngazi zote ili kulinda fedha za serikali na kukuza uchumi.
Akizungumza na watendaji wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) Prof. Mbarawa amesisitiza umuhimu wa kutopeleka fedha za mfuko wa barabara kwa halmashauri zinazoshindwa kujenga barabara bora na kuzitaka halmashauri zote kuhakikisha fedha zinazopelekwa zinawiana na miradi inayojengwa.
“Bila miundombinu ya kisasa hatuwezi kujenga uchumi tutumie fursa tuliopewa kuwatumikia watanzania kwa moyo wa uzalendo ili kukuza uchumi wa nchi,” amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Meneja wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) Bw. Joseph Haule amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa bodi hiyo inayohudumia barabara zenye urefu wa KM zaidi ya elfu 252 katika halmashauri 166 nchini imejidhatiti kuhakikisha fedha za mfuko wa barabara zinatumika kwa kazi iliyokusudiwa ili kuimarisha sekta ya uchukuzi na kukuza uchumi.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa ametembelea Bodi ya Wahandisi (ERB), Bodi ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) na Bodi ya Makandarasi (CRB) na kuagiza kurahisisha mchakato wa usajili ili kuvutia wataalam wengi wa fani za ujenzi kujisajili katika bodi hizo na kupunguza watendaji wasio na sifa.
“Sekta ya miundombinu ndio chanzo cha mafanikio ya nchi yoyote duniani hivyo fanyeni kazi kwa weledi na kuzingatia mabadiliko ya sayansi na teknolojia ili nchi ipige hatu za haraka kimaendeleo”.
Naye katibu mkuu wa wizara ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano sehemu ya ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga amezungumzia umuhimu wa bodi hizo kujitangaza katika vyuo vikuu ili kuvutia wanafunzi wengi kusoma fani za kihandisi na kuongeza idadi ya wahandisi hapa nchini.
Amezitaka wakala na bodi zinazohusika na ujenzi kuongeza ubunifu ili kutoa huduma bora na kuiwezesha serikali kufikia malengo yake kwa wakati.
Waziri Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya kukagua miradi ya ujenzi na kutoa mwongozo wa namna ya kuitekeleza kwa wakati ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO WIZARA YA UJENZI,UCHUKUZI NA MAWASILIANO