Na Mwandishi Wetu
WAKATI mgomo wa walimu umeingia siku ya tatu leo maeneo mbalimbali ya nchi, Rais Jakaya Kikwete amewataka walimu kuacha kitendo cha kuwazuia baadhi ya walimu wasiounga mkono mgomo huo ili waendelee kutoa mafunzo.
Rais Kikwete ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na wahariri kutoka vyombo anuai vya habari, ikiwa ni utaratibu wake wa kulihutubia taifa kila mwisho wa mwezi.
Amesema nyongeza ya mishahara kwa asilimia 100 wanayodai walimu hao ni kiasi kikubwa cha fedha hivyo Serikali haiwezi kukubaliana na kiwango hicho, na kuwaomba warudi katika mazungumzo ili kutafuta muafaka. Rais Kikwete pia amewataka walimu kuacha kuwatumia wanafunzi kufanya maandamano kushinikiza malipo yao kwani jambo hilo ni hatari.
“…Pengine ni mapema kulisemea hili (mgomo wa walimu) kwa vile kesho Mahakama itaamua kuhusu shauri hilo. Lakini napenda kuwahakikishia walimu kuwa tunawajali, tunawathamini na kutambua mchango wao muhimu kwa taifa letu.”
“Wakati wote tumekuwa tunashughulikia madai ya haki zao na malimbikizo mbalimbali. Madai ya safari hii ni makubwa mno, yametuzidi kimo. Athari za kuyatimiza yalivyo yataifanya bajeti ya Serikali kutumia asilimia 75 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali na kubakiza asilimia 25 kwa kuendeshea Serikali na kutimiza majukumu ya maendeleo kwa wananchi.” Alisema Rais Kikwete.
“Haitakuwa sawa. Ndiyo maana tumeshindwa kuelewana walipokataa rai hiyo na wao kusisitiza kugoma. Wakati tunaendelea kusubiri uamuzi wa Mahakama, nina maombi mawili kwa walimu: Moja, wasiwalazimishe walimu wasiotaka kugoma wafanye hivyo, wawaache waendelee na kazi. Pili, wasitumie watoto isivyostahili kujenga hoja zao. Nawasihi warudi kwenye meza ya mazungumzo.”
Mgomo wa walimu leo umeingia siku ya tatu kitendo ambacho kimezidi kuathiri shughuli za mafunzo shuleni, huku baadhi ya wanafunzi kutoka shule mbalimbali wakiandamana kwenye ofisi za Serikali wakitaka suala hilo lishughulikiwe haraka, ili wao waendelee kufundishwa shuleni.