Na Joseph Ishengoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amesema hana mamlaka ya amri kuzungumzia uraia pacha kwasababu suala hilo ni la kikatiba. Rais Kikwete alisema hayo katika Kongamano la Kwanza la Diaspora lililofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Diaspora ni lugha inayotumika kuwatambulisha Watanzania walioko nje ya nchi wanaojiendeleza kwa njia mbalimbali ikiwemo elimu. Kongamano hilo la siku mbili lenye lengo la kuelimishana, kubadilishana mawazo na kujadili fursa za uwekezaji, linaudhuriwa na wajumbe kutoka nchi 17 duniani.
“Serikali imelisikia suala la uraia pacha, lakini ni la kikatiba sio la Rais. Katiba ndio sheria mama sisi hatuna mamlaka ya amri kulizungumzia.”
Kwa mujibu wa Rais, watanzania waliowengi uraia pacha hauwakeleketi, hivyo diaspora wanaoishi nje ndio wanaostahili kulisukuma, lakini kwa sasa sauti yao bado haijasikika sana, badala ya kulizungumzia kwa nguvu, wanatumia muda mwingi kuzungumzia siasa za mitaani kwenye mitandao ya kijamii pindi wanapopata nafasi.
“Sauti yenu haijasikika sana, badala yake mnatumia muda mwingi kuzungumzia siasa za mitaani. Suala la uraia pacha liko mikononi mwa Bunge Maalum la Katiba. Kama katiba haijasema nyinyi ni rais, sheria ikitungwa haiwezi kuwapa uraia,” amesema.
Kwa mujibu wa Rais, rasmu ya Katiba iliyopo inazungumzia hadhi ya Watanzania walioko nje sio uraia. “Mnachoweza kufanya ni kushawishi wabunge wa Bunge Maalum la Katiba kukubali uraia pacha kuwa ndani ya katiba na hili sio jambo haramu, zungumzeni nao serikali haina tatizo nalo iwapo Katiba itawatambua.”
Pamoja na uraia pacha, Rais amewaomba wanadiaspora kuzingatia uwekezaji ndani ya nchi ili kuleta maendeleo ya kiuchumi, kutafuta masoko ya bidhaa ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi, kuunda umoja utakaowaunganisha na kutumia teknolojia na maalifa wanayopata nje kuendeleza taifa lao.
Kauli mbiu ya kongamano hilo ni, “Nyumbani ni Nyumbani.” Awali Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Mizengo kayanza Pinda ametaka mkutano huo kusaidia kukata kiu ya Watanzania kupata majibu ya mambo ambayo wamekuwa wakiulizia pindi wanapokutana na viongozi mbalimbali wa nchi nje ya Tanzania.