Na Joachim Mushi
KAMPUNI ya Bia ya Serengeti Breweries Ltd (SBL) inayovuma kwa bia yake ya Tusker leo mchana huu imekabidhi hudi ya sh. milioni 823 kwa Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ikiwa ni kitita cha udhamini wa Mashindano ya CECAFA Tusker Challenge mwaka huu.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa SBL, Richard Wells alisema hatua hiyo ni moja ya malengo ya kampuni yao iliyojiwekea ya kuinua soka nchini, pamoja na kuza vipaji vya mpira huo Mashariki na Magharibi mwa Afrika.
Alisema kukabidhi kwa fedha hizo katika mashindano hayo kunadhihirisha msimamo wa SBL na namna inavyowajibika kwa jamii inayowazunguka ndani na nje ya Tanzania. Alisema fedha hizo zitatumika kuratibu waandishi wa habari pamoja na mahitaji mengine ya kiutawala.
“Tunatengeneza Tusker nchini Tanzania sasa, na kinywaji hiki kinapatikana katika eneo zima la Afrika Mashariki. Tunajivunia kuwa wadhamini wakuu wa mashindano haya na tunashukuru kupewa heshima hii na CECAFA pamoja na TFF. Hii ni mara ya pili mfululizo kwa kampuni ya bia ya Serengeti kudhamini mashindano haya.
SBL mwaka jana kwenye udhamini wa mashindano hayo ilitumia kiasi cha sh. milioni 675. Timu ambazo zinatarajia kushiriki katika mashindano ya mwaka huu yanayotarajia kuanza Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Djibouti, Somalia, Ethiopia, Sudan, Zanzibar, Eritrea pamoja na Tanzania.
Wells amesema kwa kutoa kiasi hicho cha fedha na kuwa mdhamini mkuu wanaruhusiwa kutangaza bidhaa yake ya Tusker kipindi chote cha mashindano. Mshindano hayo yanatarajia kuanza Novemba 25 hadi Desemba 10, 2011.