Serengeti Boys Yatua Goa Salama

serengeti

Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 maarufu kama Serengeti Boys imetua salama jijini Goa, India kwa ajili michuano maalumu ya soka ya kimataifa kwa vijana (AIFF Youth Cup 2016 U-16) yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka nchini humo (AIFF).

Mkuu wa msafara wa timu hiyo, Ayoub Nyenzi amesema kwamba wamepokelewa vizuri na wenyeji India na leo asubuhi Mei 12, 2016 wachezaji watapumzika kabla ya baadaye saa 10.00 jioni kuanza kujifua kwa mazoezi mepesi.

“Napenda kuwajulisha kuwa timu imefika salama katika Jiji la Goa na tumepokelewa vizuri na wenyeji wetu. Kwa muda huu wa asubuhi wachezaji watapumzika mpaka saa kumi jioni wataanza program ya mazoezi,” amesema Nyenzi.

Kikosi hicho cha wachezaji 22, kiko chini ya Kocha Bakari Shime na kinaundwa na makipa, Ramadhan Kabwili, Kelvin Kayego na Samwel Brazio wakati mabeki wa pembeni ni Kibwana Shomari, Nicson Kibabage, Israel Mwenda na Ally Msengi.

Mabeki wa kati ni Issa Makamba, Nickson Job na Ally Ng’anzi huku viungo wakiwa ni Maulid Lembe, Asad Juma, Kelvin Naftari, Yasin Mohamed na Syprian Mwetesigwa na washambuliaji ni Aman Maziku, Rashid Chambo, Enrick Nkosi, Yohana Mkomola, Mohamed Abdallah, Shaban Ada na Muhsin Mkame.

Maofisa watakaosafiri na timu hiyo ni pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa TFF, Ayoub Nyenzi, Mshauri wa ufundi wa timu za vijana, Kim Poulsen, Kocha Mkuu, Bakari Shime, Kocha wa Makipa Mohamed Muharami, Daktari wa timu, Shecky Mngazija na mtunza vifaa, Edward Edward.

Michuano hiyo inatarajiwa kuanza leo Mei 12, 2016 kwa mfumo wa ligi kwa timu tano kucheza mechi nne, Tanzania itafungua dimba dhidi ya Marekani kwenye Uwanja wa Tilak Maidan, Vasco, Goa huku mchezo wa pili ukiwa kati ya wenyeji India dhidi ya Malysia Mei 15, mwaka huu.

Serengeti Boys watashuka dimbani tena Mei 17, kucheza na wenyeji India mchezo wa kwanza, Mei 19 Serengeti Boys watacheza dhidi ya Korea Kusini na mchezo wa mwisho watamaliza dhidi ya Malaysia Mei 21.

Fainali ya michuano hiyo itachezwa Mei 25 ambapo kabla ya mchezo wa fainali, utachezwa mchezo wa mshindi wa tatu katika uwanja huo huo Tilak Maidan, Vasco, Goa nchini India.

AIFF kimeandaa mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi chao kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana zitakazofanyika nchini humo mwaka 2017.