Serengeti Boys Yaapa Kuwasambaratisha Pharaohs

serengeti

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kiingilio cha shilingi elfu mbili tu (2,000) kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa kirafiki wa kimataifa kati ya Serengeti Boys (Tanzania U17) dhidi ya The Pharaohs (Misri U17).

Mchezo kati ya timu hizo za vijana utachezwa kesho Jumanne saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki na Kati, katika uwanja wa Azam Complex uliopo eneo la Chamazi jijini Dar es salaam.

Katika mchezo wa kirafiki wa awali uliochezwa Jumamosi katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Serengeti Boys waliibuka na ushindi wa mabao 2 – 1 dhidi ya The Pharaos, mabao ya Serengeti yakifungwa na kiungo Cyprian Bennedictor na Ally Hussein.

Kikosi cha Serengeti Boys kinachonolewa na makocha Bakari Shime na Sebastian Mkomwa wakishauriwa na Kim Paulsen, baada ya mchezo wa awali kimeendelea na mazoezi katika uwanja wa Karume kujiandaa na mchezo huo wa kesho.

Mchezo huo wa kirafiki ni sehemu ya maaandalizi kwa timu zote Tanzania (U17) na Misri (U17) zinazojiandaa na michezo ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika kwa Vijana mwaka 2017 zitakazofanyika nchini Madagascar.

Serengeti Boys itaanza kutupa karata yake dhidi ya Shelisheli Juni 25, 2016 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam na marudiano kuchezwa baada ya wiki moja nchini Shelisheli.