Na Mwandishi Wetu
JUKWAA la Wanawake Wajasiriamali Tanzania (TWENDE) linatarajia kufanya maonesho ya biashara za wajasiliamali ikiwa ni hatua ya pamoja kusaidiana na Serikali katika kutimiza malengo ya milenia likiwemo namba moja ambalo linalenga kuondoa umasikini.
Maonesho hayo yanayoandaliwa na TWENDE na kufanyika kila mwaka kwa miaka mitatu sasa mfululizo yanatarajiwa kuanza Oktoba 18 hadi 20 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Meneja Mradi wa TWENDE, Saphia Ngalapi lengo la tamasha hilo pia ni kuwaleta pamoja wanawake wajasiriamali wadogo, wakubwa na wale wanaochipukia ili kupata fursa ya kuuza, kuonesha na kujadili masuala ya biashara kwa ujumla.
Aidha sambamba na hilo, TWENDE inalenga kusaidiana na serikali katika kutimiza malengo ya milenia likiwemo lengo namba moja ambalo linalenga kuondoa umasikini, namba tatu kutetea haki na fursa sawa kwa wanawake, lengo namba tano kuhamasisha afya ya uzazi na lengo namba nane, ambayo ni kuendeleza uhusiano wa kudumu kwa ajili ya maendeleo ya jamii. Pia TWENDE inalenga Kukuza uzalishaji kwa wanawake wafanyabiashara na kukuza mgawanyiko wa masoko sambamba na muonekano wa wafanyabiashara wanawake katika jamii.
Kwa upande wa mwaka huu TWENDE inatarajia kuwashirikisha wanawake wajasiriamali wengi zaidi ambao wamekuwa wakifanya biashasha tofauti ili kuweza kupata fursa ya kubadilishana uzoefu na kuongeza ujuzi zaidi kibiashara. Sambamba na semina bora zitakazotolewa kwa wanawake wote ambao watapata elimu itakayotolewa wataalamu wa fani mbalimbali
“Licha ya kwamba wanawake wengi wamejikita katika sekta hii ya ujasiriamali, lakini bado wamekuwa wakikabiliawa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha kufikia malengo yao, ikiwemo elimu ya ujasiriamli na upatikanaji wa mikopo, kwa hiyo ipo haja kwa wanawake kujijengea utaratibu wa kushiriki katika fursa kama hizi zinazowajengea uwezo,” alisema Saphia Ngalapi.
Zaidi ya Wanawake Wajasiriamali Wanawake 100 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani wanatarajai kushiriki katika TWENDE mwaka huu, ampabo maonesho hayo yanakwenda sambamba na semina zitakazo tolewa kwa wanawake wote bure, kwa wale watakaoshiriki katika maonesho, na hata wale ambo watakuwa hawakupata frusa ya kuonesha na kuuza bidhaa zao.