Sekta ya Uzalishajia Bidhaa Yadoda EAC

Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki


Na Anne Kiruku (EANA)

ROBO tu ya bidhaa zinazouzwa nje ya Kanda ya Afrika Mashariki zinatokana na sekta ya uzalishaji zikiwemo bidihaa za vyakula, vinywaji, ngozi na mazao ya ngozi. Taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki jijini Nairobi imebainisha kuwa sekta hiyo ina uwezo mkubwa wa kutengeneza ajira zaidi ili kukabiliano na tatizo sugu la ukosefu wa ajira katika kanda ya Afrika Mashariki.

Taarifa hiyo inafuatia utafiti wa mwaka mmoja uliofanywa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na kuzinduliwa kwa pamoja kati ya benki hiyo, Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC).

Utafiti huo umebainisha changamoto kuu, vikwazo na mapendekezo kwa ajili ya sekta hiyo ikiwa na lengo la kuleta mapinduzi katika sekta ya uzalishaji katika kanda hiyo katika hali ya ushindani wa hali ya juu na wenye kuleta tija na faida. Utafiti huo ulihusisha nchi saba zikiwemo nchi tano wananchama wa EAC, ambazo ni Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi ambapo nyingiwe ni Ethiopia na Shelisheli.

Wakati wa uzinduzi wa ripoti, Balozi wa Korea nchini Kenya, Choi Dongyou alisema kujipatia teknolojia mpya katika sekta ya uzalishaji ni njia pekee ya kuikomboa kanda hiyo iwapo kweli inataka kupata ukuaji wa uzalishaji na kuleta tija.

“Sekta ya uzalishaji katika kanda hii ina uwezo mkubwa wa kuleta mapinduzi katika kizazi hiki,” alisema Balozi Donggyou.

Balozi huyo alisema Korea ina mfano hai juu ya suala hili na kwamba inawezekana kuleta mapinduzi katika kanda kupitia mwendelezo wa mitaji ya rasilimali watu na sekta ya uzalishaji.

Utafiti huo ulijikita kwenye uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na kilimo, hususani ni uzalishaji wa vyakula na vinjwaji, ngozi na bidhaa zitokanazo na ngozi, madawa, bidhaa toka viwanda vya nguo na mbao. Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda wa Kenya, Wilson Songa alisema taarifa hiyo itawaongoza watunga sera kuitazama upya sekta hiyo kwa lengo la kuimarisha sekta hiyo ya uzlishaji katika kanda.