Na Joachim Mushi
HATUA ya Serikali kuamua kujikita kutatua upungufu wa shule za sekondari nchini ni nzuri. Nasema ni nzuri kwa kuwa hivi sasa kuna idadi kubwa ya shule hizo ambazo zinajulikana maarufu kama sekondari za kata.
Ni kweli kwamba hata nafasi za wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza imeongezeka kwa kiasi kikubwa. Niseme wazi kwamba kama kweli shule hizi zitaangaliwa kwa karibu na kuhakikisha zinapewa nyenzo muhimu ili zifanye kazi yake kiufasaha baada ya kipindi fulani taifa litakuwa mbali kimaendeleo.
Nasema hivyo maana nchi itakuwa na wananchi wengi wenye upeo wa elimu, watakuwa wakifanya mambo yao kulingana na upeo mzuri wa elimu ambayo watakuwa wameipata kwa hatua mbalimbali.
Jambo la kujivunia zaidi shule za kata zinaongezeka kwa kasi na hata maeneo ya vijijini, ambayo awali wanafunzi walilazimika kuzifuata shule za sekondali mijini tofauti na ilivyo sasa. Elimu hii kwa sasa imewafuata walipo.
Kimsingi haya ni mafanikio makubwa. Lakini tatizo kubwa lililopo ni mzaa mkubwa tunaoufanya kwa shule nyingi za kata kwa sasa. Binafsi napenda kusema kuwa kama hali hii ikiachwa tunatengeneza bodi, ambalo litaishusha kabisa thamani ya elimu ya sekondari nchini.
Banafsi nimefanikiwa kutembelea baadhi ya shule za kata hivi karibuni Mkoa wa Rukwa, wilayani Nkasi lakini mambo niliyojionea katika shule hizo kama ndivyo yalivyo katika mikoa yote tunachokifanya ni kuua elimu ya sekondari.
Niseme wazi kwamba Wilaya ya Nkasi imejitahidi kwa kiasi kikubwa kwa ujenzi wa shule za kata ukilinganisha na shule zilizojengwa kwa miaka michache tangu kuanza kwa agizo hili la Seikali.
Lakini jambo la kusikitisha ni uendeshaji wa shule hizi. Nyingi zinaendesha kama maigizo. Nalazimika kusema maigizo kwa kuwa ni jambo la kushangaza shule inaaza na hata kufika kidato cha tatu haina walimu wa masomo ya Fizikia, Kemia, Biolojia na Kiingereza.
Shule nyingi za maeneo hayo hazina kabisa walimu wa masomo ya sayansi na hata zile zenye walimu hao hawana sifa ya kufundisha. Nasema hawana sifa kwa kuwa nimetembelea baadhi ya shule na kukuta zinafundishwa masomo kama Hisabati na vijana waliomaliza kidato cha nne.
Vijana hawa hawana mbinu zozote za ufundishaji, wanafanya hivyo kwa kutumia elimu ndogo na uzoefu walioupata wakiwa madarasa ya chini. Wapo ambao wanafundisha kidato cha kwanza hadi cha nne. Hebu tujiulize mwanafunzi wa kidato cha nne kwe anaweza kumudu madarasa manne kufundisha somo ambalo hajafuzu kuwafundisha wengine?
Hili ni tatizo kubwa, upo uwezekana baadhi ya wanafunzi wakaendelea kudanganyana wanasoma sekondari lakini akimaliza miaka yake minne shuleni hapo anatoka mtupu, kwamba huwezi kumtofautisha yeye na mwanafunzi wa darasa la saba. Hivi ni vichekesho.
Elimu ya kidato cha kwanza hadi cha nne hufundishwa kwa lugha ya Kiingereza, hili linajulikana wazi, hivyo kwa mantiki ya kawaida utaona kuwa somo la Kiingereza ni muhimu sana kwa wanafunzi wa sekondari. Chakushangaza nimetembelea baadhi ya shule hizi na kukuta hazina kabisa walimu wa Kiingereza.
Wanafunzi wanasoma lakini hawafundishwi somo la Kiingereza, sasa kwa hali ya kawaida mwanafunzi kama huyu ataweza kulielewa vizuri somo hili na kulitumia kama lugha ya maelekezo katika masomo mengine? Hii ni ajabu. Lakini amini usiamini ndivyo inavyotokea katika shule zetu ya kata.
Wanafunzi hawafundishi kabisa baadhi ya masomo lakini katika mitihani yao ya mwisho watalazimika kuyafanyia mitihani masomo hayo, watu kama hawa watajibu nini katika mitihani yao ya mwisho zaidi ya kuandika ‘madudu’? Je, kama mwanafunzi atasoma hadi kidato cha nne lakini hakufundishwa somo la Kiingereza, Baioloji, Fizikia ama Kemia utamuita muhitimu wa kidato cha nne?
Nimetembelea na kuona shule inaanzishwa hadi inafikisha kidato cha nne kaina bodi ya shule, chombo ambacho ni muhimu katika kuangalia utendaji wa shule na maendeleo kwa jumla. Shule inaanzishwa haina ofisi za walimu, maktaba, madarasa ya kutosha, stoo wala nyumba za walimu.
Ni ukweli wa mambo kwamba kama tutaendelea kujenga shule hizi na kuziacha katika mazingira kama niliyoyaona tutakua tunaandaa kundi la mbumbumbu bila kujielewa. Nasema hivyo maana tutakuwa na kundi la watu wanajiita wameitimu kidato cha nne lakini hawana chochote vichwani mwao. Kwamba itafika mahali huwezi kumtofautisha muhitimu wa kidato cha nne na yule wa darasa la saba. Siasa isitumike kuua elimu ya sekondari.