Seith Kamuhanda Amfagilia Rais Kikwete Kuteuwa ‘Majembe’

Seith Kamuhanda

Na Magreth Kinabo – MAELEZO

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Seith Kamuhanda  amempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuwateua viongozi ambao ni majembe (wachapakazi) kuiongoza wizara hiyo huku akisema ni watendaji wenye uwezo wa hali ya juu.

Viongozi walioteuliwa kuongoza wizara hiyo ni Sihaba Nkinga ambaye ni Katibu Mkuu wa sasa na Naibu Katibu Mkuu wake ni Profesa Elisante ole Gabriel Laizer.

Kauli hiyo imetolewa leo na Kamuhanda wakati akiwaga viongozi wa wizara hiyo ambapo pia aliwasisitiza kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuhakikisha huduma wanazozitoa  kupitia sekta za habari, vijana, utamaduni na michezo zinawafikia wananchi.

“Leo ni siku ya furaha kwangu kwa sababu ninaacha majembe mawili ya uhakika. Ninawaomba muwape ushirikiano ili walime vizuri. Ni wizara ngumu kwa sababu inagusa Watanzania wote,” alisema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa sasa Sihaba alisema anamshukuru Kamuhanda kwa kumfundisha kazi katika maeneo mbalimbali ya sekta za wizara hiyo.

“Nimekaa katika kiti hiki bila ya yeye nisingeweza kukaa katika kiti hiki bado ataendelea kuwa msaada kwangu kwa kuwa wizara inagusa jamii,” alisema Katibu Mkuu Sihaba huku akimwomba aendelee kutoa msaada katika wizara hiyo.

Aidha Katibu Mkuu huyo alisema atajitahidi kuongoza wizara ili iendelee kuwa watoto wa familia moja kama ilivyoachwa na Kamuhanda. Naye Naibu Katibu Mkuu  Profesa Laizer alisema anamshukuru Kamuhanda kwa ushirikiano aliowapo, pia aliongeza kuwa kufanya kazi kwake vizuri kutokana na ushirikiano huo ukiwemo wa wakurugenzi, viongozi wa taasisi na watumishi wa wizara hiyo.

“Kazi kubwa niliyonayo ni kumsaidia Katibu Mkuu. Nitawasaidia ili tupate Matokeo Makubwa Sasa. Tutajitahidi tusikuangushe,” alisisitiza Profesa Laizer huku akisema wao ni majembe lakini yeye ni shoka na ametoka katika wizara hiyo kwa heshima.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya menejimenti ya wizara hiyo Profesa, Hermans Mwansoko alimpongeza Kamuhanda kutokana na utendaji kazi wake wakati akiiongoza, ambapo alisema ameiacha katika hali ya umoja na mshikamano huku akiwajali watumishi hususan wa ngazi za chini.