Waandishi wa habari wakichukua matukio katika mkutano huo wa kutangaza mshindi mapema leo katika ofisi za SBL Temeke Jijini Dar es salaam. |
KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL) imetoa zawadi ya gari aina ya Heicher lenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 50 kwa MM Group, ambaye ni msambazaji wa kanda aliyeibuka msambazaji anayeongoza katika kipindi cha kwanza cha nusu mwaka huu wa fedha 2017.
Kampuni ya MM Group ambayo ina makao yake wilayani Mpanda Mkoa wa Katavi iliwashinda wasambazaji wengine 85 walioshiriki kwa ajili ya kupata zawadi hiyo ya kipekee. Akiendesha hafla hiyo ya makabidhiano iliyofanyika katika makao makuu ya SBL Temeke, Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mauzo wa SBL, Alain Tayo alimpongeza mshindi huku akithibitisha kujikita kwa kampuni hiyo ya bia katika kutambua juhudi zinazofanywa na wateja wake katika kuunga mkono ukuaji kwa kampuni.
“Wakati tunapongeza mchango wa MM Group kwa kuongoza na kushika nafasi ya juu katika kipengele chake kulikomwezesha kupata zawadi hii, tunatambua pia kazi nzuri inayofanywa na wasambazaji wengine, wateja na hali kadhalika wadau wetu. Kupitia uungwaji mkono huu wa dhati, SBL imekua katika uzalishaji na kufikia kiwango cha juu katika sekta ya uzalishaji bia ndani ya nchi na hata katika ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Tayo.
Akitoa wito kwa wasambazaji wengine wa SBL kuiga mfano wa MM Group, Tayo aliwahahakishia washirika wa SBL kibiashara wakiwamo wasambazaji na wateja kwamba SBL itaendelea kuwaenzi na kusikiliza mahitaji yao.
“Tunawashukuru wadau wetu wote kwa kuzingatia kwamba wamekuwa pamoja nasi katika katika safari yetu ndefu na ya mafanikio kibiashara”, alibainisha Tayo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa MM Group Joseph Chanika, wakati akiishukuru SBL kwa zawadi hiyo, aliwapa changamoto wasambazaji wengine kuendesha na kuenenda na ukaribu wa SBL kwa kufanya kazi kwa bidiii ili kufuzu kwa ajili ya tuzo kama hiyo.
“Naishukuru sana SBL kwa kuheshimu ahadi yake na kunituza gari hili Heicher. Hili gari ni zana muhimu katika biashara yangu ambayo itaniwezesha kukuza shughuli zangu za usambazaji wa bidhaa za SBL,” alisema Bw Joseph Chanika kwa bashasha.