KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL) leo imetoa msaada mifuko ya saruji 500 yenye thamani ya shilingi milioni 10 kwa wahanga wa janga la tetemeko la ardhi lililotoa mkoani Kagera. Msaada huo ni kuitikia wito wa serikali kwa mashirika, watu binafsi na watu wenye mapenzi mema wa kujitoa kusaidia wahanga wa tukio hilo.
Akizungumza katika tukio la kukabidhi msaada huo katika Ofisi ya Mkuuu wa Mkoa wa Kagera mjini Bukoba, Meneja Usalama wa SBL, Sebastian Kalugulu aliwapa pole wahanga wa tetemeko hilo kwa kuwahakikishia kwamba SBL kila mara iko tayari kusaidia pindi inapohitajiwa na jamii.
“”Tunatoa pole ya dhati na masikitiko yetu kwa wahanga wa tetemeko la ardhi na tunawaombea majeruhi wote wapone haraka,” alisema Kalugulu, na kuongeza kwamba SBL inaungana na watu wengine wenye mapenzi mema kutoa msaada wa kibinadamu kwa ajili ya kuwasaidia kuhimili kadhia iliyowapata na kurudi katika shughuli zao kawaida.
Kalugulu alithibitisha tena kwamba kampuni hiyo ya bia imejikita katika kuunga mkono serikali na watu binafsi wenye mapenzi mema, mashirika na makampuni katika kuisaidia jamii katika maeneo SBL inapoendesha shughuli zake.
“Ni matumaini yetu kwamba msaada huu utachangia katika michango iliyokwishatolewa na wasamaria wengine na kwamba itawawezesha wahanga hao kujenga miundombinu iliyoharibika na hata kuboresha maisha yao.”
Akizungumzia mchango uliotolewa na SBL, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu alisema kwamba msaada huo unachangia katika michango mingine kutoka kwa watu wenye mapenzi mema kutoka ndani, mikoani na kimataifa ambao kmwa ukarimu waliitikia wito wa serikali wa kusaidia.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa atahakikisha kuwa msaada huo unaenda kwenye lengo lililokusudiwa na kutoa wito kwa watu zaidi kuendelea kuwasaidia wahanga.