Kwa mara ya kwanza katika historia, mwanamke ameteuliwa kuwa katibu mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), shirikisho ambalo kwa kiwango kikubwa limetawaliwa na wanaume.
Bi Fatma Samba Diouf Samoura kutoka Senegal, ndiye katibu mkuu mpya. Atasimamia shughuli za kila siku katika shirikisho hilo ambalo kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa limekabiliwa na tuhuma za ulaji rushwa.
Ni mwanadiplomasia aliyehitimu ambaye kwa sasa amekuwa akihudumu kama mratibu wa masuala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa nchini Nigeria.
Amefanya kazi UN kwa miaka 21.Bi Samoura amesema ni fahari kubwa sana kwake kuteuliwa kwenye wadhifa huo.
Tangazo hilo limefanywa na rais wa FIFA Gianna Infantino katika kongamano kuu la FIFA linaloendelea Mexico. Aliyekuwa katibu mkuu wa FIFA Jerome Valcke alipigwa marufuku kutojihusisha na shughuli zozote za soka kwa miaka 12 mapema mwaka huu.