Rene Angelil, mume wa mwanamuziki mashuhuri duniani Celine Dion, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 73, mwanamuziki huyo ametangaza. Bw Angelil, aliyemuoa Dion mwaka 1994 na wakajaliwa watoto watatu, amekuwa pia akihudumu kama meneja wake. Alifariki akiwa nyumbani kwao Las Vegas baada ya kuugua saratani.
Dion alichukua likizo kutoka kwenye muziki kwa vipindi viwili ili kumtunza Angelil baada yake kupatikana na saratani ya koo mwaka 2000. Bw Angelil alizaliwa mjini Montreal mwaka 1942.
Baada ya kuwa meneja wa makundi kadha nchini Canada, aliombwa na wazazi wa Dion awe meneja wake mwanamuziki huyo alipokuwa na umri wa miaka 12 pekee. Mwaka jana, Dion aliambia gazeti la USA Today kwamba alikuwa akijiandaa kwa kifo cha mumewe.
Gazeti la Montreal Gazette linasema Bw Angelil aliweka rehani nyumba yake ili kupata pesa za kufadhili albamu ya kwanza ya mwanamuziki huyo, Dion amerekodi albamu 25 studioni na ndiye mwanamuziki wa tano kwa kulipwa pesa nyingi zaidi, utajiri wake ukikadiriwa kuwa $630m (£437m).
Mwaka 1999, wimbo wake My Heart Will Go On, uliotumiwa katika filamu ya Titanic, ulishinda tuzo mbili za Grammy. Amekuwa akitumbuiza mara kwa mara katika ukumbi wa The Colosseum, Caesars Palace mjini Las Vegas tangu 2003.
Alianza tena kutumbuiza mashabiki wake mwaka jana baada ya kupumzika mwaka mmoja kumtunza Bw Angelil, ambaye aliacha kuwa meneja wake 2014.