Samuel Sitta Awaita Viongozi wa UKAWA Waigizaji
Na Benedict Liwenga, MAELEZO – Dodoma
MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta amewaadaa baadhi ya viongozi wanaojiita UKAWA kwa taarifa yao ya kutaka kumfikisha Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa kwa kuendeleza mchakato huo wa Katiba. Kauli hiyo imetolewa Septemba 12, 2014 mjini Dodoma na Sitta kufuatia baadhi ya viongozi hao, kudai kuwa watampeleka katika mahakama hiyo.
Sitta ameeleza kuwa baadhi ya viongozi wa UKAWA wanakipaji cha uigizaji huku akieleza kuwa walipokuwa bungeni wakati wa mchakato wa kupiga kura za siri, viongozi hao walizifanya kura hizo kuwa wazi na baadaye kuja na kauli kuwa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea sasa sio halali lihairishwe.
“Juzi Mhe. Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amekutana nao mara mbili kwa muda wa saa Saba na katika kukutana huko wakafikia maafikiano, lakini siku moja baadaye wao wamekana yote waliyokubaliana hapa mjini Dodoma, kwa hiyo ni vyema wananchi wakawapima hawa watu,” alisema Sitta.
Aidha, Sitta alisema kuwa wananchi na viongozi wanatakiwa kujua kuwa mchakato wa bunge Maalum la Katiba sio jambo la mzaha na wao hawapo hapo bungeni kwa mzaha mzaha. “Mimi nawaambia kuwa hapo mwakani watakaposhindwa uchaguzi basi warejee katika fani zao ambazo Mwenyezi Mungu kawajalia,” alisema Sitta.