Samia Awataka Wakadiriaji Majenzi Kuwa Waadilifu

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan mwenye wa kwanza kushoto akipata maelezo kutoka kwa Mkadiliaji majenzi wa kampuni ya ujenzi ya  Advent Construction Limited Bahati Mbambe katikati alipotembelea banda hilo wakati wa uzinduzi wa mkutano wa kimataifa wa wakadiriaji majenzi Afrika uliofanyika leo jijini Dar es salaam na wa kwanza kulia ni Meneja Mwendeshaji wa kampuni hiyo Bi. Isabel Mwangangi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan mwenye wa kwanza kushoto akipata maelezo kutoka kwa Mkadiliaji majenzi wa kampuni ya ujenzi ya Advent Construction Limited Bahati Mbambe katikati alipotembelea banda hilo wakati wa uzinduzi wa mkutano wa kimataifa wa wakadiriaji majenzi Afrika uliofanyika leo jijini Dar es salaam na wa kwanza kulia ni Meneja Mwendeshaji wa kampuni hiyo Bi. Isabel Mwangangi.

Na Frank Shija-Maelezo

WATAALAMU wa Ukadiriaji Majenzi wameelezewa kuwa ni kada muhimu katika kukabiliana na tatizo la rushwa pamoja na matumizi mabaya ya rasilimali za umma katika sekta ya ujenzi dunia kote.

Hayo yamebainishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Hassan Suluhu wakati akimuwakilisha Rais John Pombe Magufuli katika hafla ya uzinduzi wa mkutano wa Kimataifa wa Wakadiriaji Majenzi barani Afrika uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

“Ni matumaini yetu kwamba umuhimu wa huduma zinazotolewa na Wakadiriaji Majenzi zina mchango mkubwa sana kwenye mapambano dhidi ya rushwa katika sekta ya ujenzi”. Alisema Makamu wa Rais.

Mkutano huo wenye kauli mbiu isemayo “Kuelekea kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu – Mchango wa huduma za Wakadiriaji Majenzi” umekuja wakati muafaka ambapo Tanzania inahitaji kupata uzoefu kutoka kwa Wataalamu kutoka nje ya nchi kwa kuwa ipo mbioni kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi na imekusudia kuwatumia Wataalamu wa ndani zaidi.

Aliongeza kuwa kutokana na umuhimu wa Wakadiriaji Majenzi hasa katika kuleta uwazi Serikali itawatumia wataalamu hao katika kutekeleza mipango yake ya ujenzi wa miundombinu iliyopangwa kutekelezwa ambapo ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya kati kwa Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge) na ujenzi wa Bomba la mafuta kutoka Bandari ya Tanga hadi Uganda ujenzi unaotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais alipata fursa ya kutembelea baadhi ya mabanda ya Taasisi zinazojihusisha na ujenzi ambapo alitoa pongezi kwa Baraza la Ujenzi la Taifa (NCC) kwa jitihada zake katika utatuzi wa migogoro itokanayo na sekta ya ujenzi, na kuwashauri kuongeza bidii katika kuhakikishi inatoa huduma zake maeneo mengi zaidi.Huduma zingine zitolewazo na baraza hilo ni pamoja na ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa miundombinu pamoja na majengo, utafiti na ushauri wa kitaalamu.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa mkutano huo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa rai kwa Wakadiriaji Majenzi kuwa waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuepusha hasara zitokanazo na udanganyifu katika miradi ya ujenzi.

Aliongeza kuwa ni bora kuwa na Wakadiriaji Majenzi wachache ambao ni waadilifu kuliko kuwa na lundo la wataalamu hao wasio waadilifu na kuongeza kuwa uadilifu ndiyo sifa kuu katika taaluma yeyote.

“Bora kuwa na Wakadiriaji wachache wenye sifa ya uadilifu kuliko kuwa na Wataalamu hao wengi wasio kuwa na maadili”. Alisema Profesa Mbarawa.

Kwa upande wake Rais wa Taasisi ya Ukadiriaji Majenzi Tanzania (TIQS) Samuel N. Marwa ameiomba Serikali kuwatumia Wataalamu wa Ukadiriaji Majenzi kwa kuwa wataalamu hao ni muhimu na kutapunguza mianya ya rushwa.
Wakadiriaji Majenzi wamejipanga kuhakikisha wanafanya majukumu yao ili kutekeleza malengo ya manedleo endelevu na kuongeza kuwa karibu sekta zote zinahitaji ujenzi akitolea mfano wa huduma ya Afya kwa kusema ili maendeleo katika sekta hiyo yapatikane ni lazima kuwepo na majengo kwa ajili ya huduma hiyo.
“Wakadiriaji wa Majenzi wakitumika vizuri kutapunguza sana mianya ya rushwa kwa kuwa kabla ya hatua ya kumpata mkandarasi tayari utakuwa umeshajua gharama halisi ya ujenzi husika”
Utalaamu wa Ukadiriaji Majenzi unaweka uwazi katika mchakato mzima katika shughuli za miradi ya ujenzi.