Siku chache baada ya mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania Mbwana Samatta kutangazwa mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani, kocha mkuu wa timu ya taifa ya Charles Boniface Mwasa amemteua Samatta kuwa nahodha mpya wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Samatta anakuwa nahodha mpya wa Stars akichukua nafasi ya mkongwe Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye amekuwa nahodha wa kikosi hicho kwa muda mrefu tangu aliporithi kijiti hicho kutoka kwa Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’.
Maamuzi hayo ya Mkwasa yamekuja kutokana na star huyo wa bongo kukidhi vigezo vyote vya kuwa nahodha wa timu ya taifa kwa kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja sambamba na kujituma kila anapokuwa kwenye timu ya taifa uwezo wake wa kuzungumza na kila mchezaji lakini pia kupata mafanikio makubwa kwenye soka la Afrika.
Mkwasa amesema kuwa anafikiri ni mabadiliko ya kawaida, baada ya kupata tuzo na heshima kubwa Afrika, na wameamua kumuongezea majukumu mengine ili aweze kutuongozea timu yetu ya taifa na watanzania kwa ujumla ameweza kuiongoza vizuri TP Mazembe na kuwa mabingwa wa Afrika tumeona tumpe fursa hii ili awaongoze wenzake kwa hizi mechi za AFCON zilizobaki.
“Ingawa tumechelewa lakini hatuna jinsi, kwahiyo tumempa nafasi hiyo anasaidiwa na John Bocco, Cannavaro tunampa jukumu la kusimamia timu ya CHAN lakini tunamtafutia nafasi nyingine katika Stars”.
Kupewa unahodha kwa Samatta hakumaanishi kwamba Cannavaro amepoteza sifa na vigezo vya kuwa nahodha bali ni kuthamini heshima ambayo Samatta ameliletea Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla kwa kuwa mchezaji wa kwanza kutwaa tuzo hiyo kwenye ukanda huu.
Cannavaro bado ataendelea kuwa kiongozi wa Stars kutokana na uzoefu alionao kwenye timu hiyo lakini pia kutokana na mafanikio aliyoiletea Tanzania kupitia Stars pamoja na kudumu kwa kiwango chake kwa muda wote ambao amekuwa akikitumikia kikosi cha timu ya taifa.