KAMPUNI ya Simu nchini Tanzania (TTCL) sasa imerahisisha upatikanaji wa vocha zake baada ya kuingia makubaliano kuishirikiano na benki 13 nchini zinazotoa huduma zake pia kwa kupitia simu za mkononi (Mobile Banking) ambapo sasa mteja wa TTCL ataweza kuongeza salio kupitia simu yake ya mkononi (TTCL top-up).
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Meneja Mipango na Mauzo wa TTCL, Benjamin Bizere alisema huduma hiyo ya kununua salio kwa njia ya simu kupitia mabenki 13 imeanza kufanya kazi hivi sasa hivyo mteja wa TTCL anaweza kununua salio lake popote alipo kwa kutumia simu yake.
Alisema TTCL imeingia makubaliano ya kiushirikiano katika uuzaji wa muda wa maongezi kwa benki za Standard Chartered, Akiba Commercial (ACB), Tanzania Postal Bank (TPB), Exim Bank, Dar Es Salaam Community Bank (DCB), Mkombozi Bank, KCB Bank pamoja na Bank of Africa ambazo wateja wa beki hizo wanaweza kununua salio kupitia simu zao popote walipo kwenye akaunti zao.
“…Jumla ya benki 13 zimeingia ubia wa kibiashara na TTCL kwa ajili ya kuuza vocha za TTCL kupitia benki zao…hapo juu nimetaja majina ya benki zote ambazo zinatumika kwa ajili ya kufanya miamala mbalimbali ikiwemo TTCL TOP-UP,” alisema Bw. Bizere.
Akifafanua zaidi juu ya huduma hiyo Mkuu wa Mauzo wa TTCL, William Chamla alisema huduma ya TTCL TOP-UP na Mobile banking ni njia ambayo TTCL imeanzisha kwa wateja wake kwa ajili ya kuongeza salio la muda wa maongezi kwa simu za mezani, mkononi na kununua vifurushi vya intaneti hivyo mteja ataweza kununua salio lake muda wowote na popote.
“…Mteja atakayenufaika na huduma hii ni yule mwenye akaunti ya benki, na amejisajili katika huduma ya kibenki kupitia simu ya mkononi yaani ‘mobile banking’. Hata hivyo alisema ili kuwarahisishia upatikanaji wa huduma kwa wateja wa wao vocha za TTCL pia zinapatikana katika vituo vya Maxmalipo na Selcom ‘wireless Point’ na kwenye Ofisi za TTCL, pamoja na vituo vya huduma kwa wateja ambako viko katika kila mkoa na wilaya.