Sakata la Escrow; Rais Kikwete Amfukuza Uwaziri Prof Tibaijuka

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alipozungumza na waandishi wa habari.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alipozungumza na waandishi wa habari.

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amemfukuza kazia Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kwa kukiuka sheria ya maadili ya umma kwa kile kupokea kiasi kikubwa cha fedha toka kwa mfanyabiashara James Rugemalira wa VIP Engineering & Marketing.

Rais alitengua uteuzi wa Waziri Prof. Tibaijuka jana alipokuwa akizungumza na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam na kuongeza kuwa amemuweka kiporo Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Muhongo ambaye maazimio ya bunge juu ya uchunguzi wa sakata la Escrow yalimtaka avuliwe madaraka.

“…Waziri wa ardhi (Prof. Tibaijuka), tumekaa nae na kuzungumza. Pesa hizi ni za nini na kwa ajili gani na amesema ni za shule, mengi yameelezwa. Maswali makubwa kwa nini hazijaenda shuleni moja kwa moja na zikawa kwa jina lake, akasema ndo masharti ya mtoaji, tumelitafakari sana na tumeona msingi mkubwa wa kimaadili kuhusu kupokea hizi pesa, tumeshazungumza nae na tumemwambia atupe nafasi tumteue mwingine,” alisema Rais Kikwete.

Akizungumzia kuhusu maazimio mengine ikiwa ni pamoja na la kumtaka kuwawajibisha wajumbe wa bodi ya TANESCO alisema uzuri bodi yenyewe imemaliza muda wake na tayari ameanza mchakato wa bodi mpya na inatarajiwa kutangazwa siku chache zijazo. Akizungumzia kumuwajibisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini alisema ni mtumishi wa umma, hivyo kuna taratibu zake za kumuwajibisha hivyo ameshaagiza zianze.

“…Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameshajiuzulu na amesema amebeba dhamana hiyo pia kwa niaba ya waliojiuzulu. Waziri wa nishati na madini tumemuweka kiporo, kuna uchunguzi nimeagiza ufanywe na nikipata majibu nitafanya uamuzi, tume ya maadili pia wanafanya kwa ajili ya kupata maamuzi kwa misingi ya haki,” alisema Rais Kikwete.

Akifafanua juu ya maazimio ya bunge alisema serikali imayakubali na kulipongeza bunge kwa hatua hiyo. Alikiri kuwa watuhumiwa wanatoka CCM ila sio kwamba CCM inaridhia vitendo hivyo. “…Ntashangaa mbunge kulipinga hili eti kisa tu yuko CCM, bunge wengi ni CCM, kama ni kweli walikuwa hawataki hakuna azimio lingepita? Na kuna baadhi ya wabunge wa CCM waliudhika na maovu haya, wenzetu wanatafuta sifa laini kwa jambo ambalo ni letu sote.”

“Niwahakikishie mimi na wenzangu serikalini hatuna upungufu wa dhamira katika kutimiza maazimio ya bunge. Kutaifisha mitambo ya IPTL, tunahimiza sekta binafsi kuwekeza, tunapotaifisha habari tunayopeleka si nzuri, sisi tuliotaifisha mwanzo siku hizi tunasema hatuna sera ya ujamaa hivyo waje kuwekeza. Watasema wale jamaa wamerudia tena wanataifisha.”

“…Haya ya kutaifisha yananipa wasiwasi Kuhusu uwazi wa mikataba na mapitio, tutafanya na lipo moja tutafanya kuhusu usiri wao wa biashara, kuweka wazi zinaweza kutumiwa na wapinzani wa kibiashara, hivyo tutaangalia namna ya kulifanya.” alisema.

Akizungumza juu ya azimio la rais kuunda tume ya kijaji kuwachunguza majaji (Mujulizi na Lwangisa), alisema suala hilo amelipokea lakini utaratibu wa kisheria kushughulikia linatakiwa lianzie kwenye mahakama na sio kwa rais au bunge.

“…Nilichosema tumwachie jaji mkuu na wakiridhika watakuja kwa raisi endapo wataridhika wahusika wamekosa sifa. Kuhusu mabenki kuwekwa kama zinatakatisha fedha, pendekezo uchunguzi ufanyike ni pendekezo zuri na intelligence unit ndio watakaofatilia. Serikali iandae muswada wa sheria ulioleta TAKUKURU, ni wazo zuri, Mchakato wa kufanya mageuzi TAKUKURU tumeuanza tangu 2008. Sheria ya kwanza ya PCCB ilikua na makosa manne tu ya rushwa tukayaongeza mpaka 24,” alisema Kikwete.