SAFU ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) sasa imekamilika baada ya kupatikana wajumbe wa Kamati Kuu (CC), mjini Dodoma jana. Kwa mujibu wa taarifa ambazo mtandao huu umezipata waliochaguliwa katika chombo hicho kikuu cha uamuzi ndani ya CCM; kutoka Tanzania Bara ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma, Alhaji Adam Kimbisa, Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa na Mbunge wa Viti Maalum, Pindi Chana.
Kutoka Zanzibar ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani, Dk Salim Ahmed Salim, Waziri wa Ulinzi, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi. Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri wa zamani wa Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Maua Abeid Daftari pamoja na Khadija Aboud. Wajumbe hao wapya wanaunda Kamati Kuu pamoja na wengine wanaoingia kwa nyadhifa zao.