SAFA yaomba radhi na kuondoa rufaa CAF

Mashabiki wa Timu ya Taifa ya Afrika Kusini katika moja ya ushangiliaji wa timu yao

CHAMA cha Soka cha Afrika Kusini (Safa) kimefuta rufaa yake iliyokuwa na utata kwa Shirikisho la Soka la Afrika Caf kuhusiana na utaratibu wa kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika.
Safa pia imeomba radhi kwa nchi kutokana na timu yao ya taifa ya soka Bafana Bafana kushindwa kufuzu kucheza katika mashindano yajayo ya Kombe la Mataifa ya Afrikas.
Chama hicho cha soka cha Afrika Kusini ambacho kinasakamwa sana nchi kwao hivi sasa, kimeipongeza Niger kwa kufuzu katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatano.
Licha ya kushindwa kufuzu, kocha wa Bafana Bafana Pitso Mosimane ataendelea na kazi yake ya kuifundisha timu hiyo.
Maafisa wengine walio katika timu hiyo watachunguzwa kwa kumpa taarifa za uongo kocha huyo kuhusiana na hali itakavyokuwa kutokana na nchi hiyo kwenda sare ya kutofungana na Sierra Leone katika mechi ya mwisho ya kuamua nani atafuzu kwa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Safa iliwasilisha rasmi rufaa yake wiki iliyopita kwa Caf wakipinga utaratibu wa kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika unaotumika kuzitenganisha timu zinapokuwa zimefungana kwa kila kitu.
Lakini baada ya kushutumiwa vikali na Waziri wa Michezo Fikile Mbalula na wapenda soka kwa ujumla kwa kuipinga Caf, Safa imeamua kuondoa rufaa yake na kuomba radhi.

-BBC