KAMATI ya Siasa Ulinzi na Usalama ya nchi zinazounda Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) imesema ina imani kuwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu nchini Zimbabwe utakuwa huru na wa haki.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo juzi tarehe 20 Mjini Pretoria mara baada ya kumalizika kwa kikao cha siku moja cha kamati ya SADC iliyokutana chini ya uenyekiti wa Tanzania kuzungumzia hali ya kisiasa katika Jamhuri ya Watu wa Congo (DRC), Madagascar na Zimbabwe.
“Ni uchaguzi ambao unachangamoto zake kutokana na muda wa kujitayarisha na pia gharama za uendeshaji wake lakini tuna amini utakua uchaguzi huru na wa haki” Rais Kikwete amesema wakati akijibu maswali ya waandishi mara baada ya kikao cha wajumbe wa kamati ya siasa, ulinzi na usalama ya SADC.
Nchi zinazounda kamati hii ni Tanzania ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati hii, Msumbiji ambayo ndiye Mwenyekiti wa Jumuiya ya SADC, Afrika Kusini na Namibia ni wajumbe katika kamati hii.
Akisoma taarifa ya pamoja ya viongozi katika mkutano wa waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya SADC Bw. Toma Salomao amesema vyama vyote vya siasa vinavyotarajiwa kushiriki uchaguzi mkuu ujao nchini Zimbabwe vimeahidi kufanya uchaguzi huo kwa amani na kwamba kikao kinaamini wagombea watasimamia utekelezaji huo.
Maswala mengine yaliyozungumzwa katika kikao hicho ni hali inavyoendelea DRC baada ya kupelekwa kwa jeshi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani ambapo Tanzania pia imepeleka kikosi chake kama wajibu wake katika Umoja wa Mataifa.
Pamoja na kikao kupongeza juhudi za kikosi cha kulinda amani nchini Congo, kikao kimezitaka pande mbili zinazopigana katika mgogoro huo ambao ni serikali na kikosi cha waasi cha M23 kusitisha mapigano na kurejea kwenye meza ya mazungumzo ili kuondoa tofauti zao.
Na kuhusu Madagascar kikao kimeitaka tume ya uchaguzi nchini humo kutoa ratiba mpya ili matayarisho ya uchaguzi yaanze kufanyika.
Rais Kikwete amerejea Dar Julai, 2013
Imeandaliwa na: Premi Kibanga, Mwandishi Msaidiziwa wa Rais,
Pretoria- Afrika Kusini.