KIUNGO wa timu ya Coastal Union, Sabri Ramadhan ‘China’ amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Septemba katika Ligi Kuu ya Vodacom.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Dar es Salaam na Ofisa Habari wa TFF, China amechaguliwa baada ya kupata pointi nyingi kwenye mechi alizocheza kwa mwezi huo. Baadhi ya mechi alizopata pointi nyingi ni dhidi ya African Lyon na JKT Ruvu Stars.
Wambura alisema katika mechi namba 27 dhidi ya Lyon iliyochezwa Septemba Mosi kwenye Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam na timu yake kushinda bao 1-0 alipata pointi 85 kati ya 100.
Aidha ameongeza kuwa mchezaji huyo pia alipata pointi 89 kwenye mechi namba 33 dhidi ya JKT Ruvu Stars iliyochezwa Septemba 5 mwaka huu Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam. Coastal Union ilipoteza mechi hiyo kwa mabao 3-0.
Kwa kuibuka mchezaji bora wa Septemba, China atazawadiwa kitita cha sh. 600,000 kutoka kwa mdhamini wa ligi hiyo, kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom
Mchezaji bora wa Agosti alikuwa kiungo wa Polisi Dodoma, Ibrahim Massawe ambaye kwenye mechi namba 4 ya ligi hiyo dhidi ya African Lyon iliyochezwa Agosti 20 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma alipata pointi 93 ambazo hazikufikiwa na mchezaji yeyote kwa Agosti.
Katika hatua nyingine chama cha Mpira wa Miguu Poland (PZPN) kimetuma maombi ya kupatiwa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya mchezaji Khatib Waziri Mzee ili aweze kucheza mpira wa miguu nchini humo.
Taarifa zinasema PZPN imetuma maombi hayo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ili kumwezesha mchezaji huyo kuichezea timu ya LUKS Wierzbiecice ambayo hata hivyo haikuelezwa iko ligi ya daraja gani nchini humo.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa PZPN, Zdzislaw Krecina, Mtanzania huyo aliyezaliwa Julai 30, 1974 ameombewa hati hiyo kama mchezaji wa ridhaa kwa maelezo kuwa hakuwahi kusajiliwa na klabu yoyote nchini. TFF inafanyia kazi maombi hayo na hati hiyo itatolewa mara baada ya taratibu husika kukamilika.