Na Joachim Mushi
KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imemvua nafasi zote za uongozi ndani ya chama, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe pamoja na viongozi wengine wawili wa juu wa chama hicho kwa tuhuma za kutaka kukiangamiza chama kwa siri.
Zitto pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Dk. Kitilla Mkumbo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwiganda na mfanyakazi mmoja wa chama hicho Makao Mkuu ya chama wamevuliwa nafasi zao zote baada ya kutuhumiwa kuunda ‘Mtandao wa Ushindi’ waliouita Mkakati wa Mabadiliko 2013 kikichafua chama na viongozi wake wakuu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na Chadema Makao Makuu na kusainiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake, Dk. Wilbrod Slaa- viongozi hao wanaandikiwa barua ya kutakiwa kujieleza na kusema kwanini wasifukuzwe ndani ya chama kwa kitendo walichofanya.
Taarifa hiyo inadai ‘Mtandao wa Ushindi’ ulioanzishwa na viongozi hao waliouita Mkakati wa Mabadiliko 2013 na kuuendesha kwa siri haukuwa na nia njema na chama bali kutaka kukiua chama jambo ambalo Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana imelipinga vikali.
Uamuzi huo mzito ndani ya Chadema ambao ni matokeo ya Kikao cha Kamati Kuu iliyokutana kwa siku tatu mfululizo jijini Dar es Salaam umebainisha Zitto (ambaye anadaiwa kuwa muhusika mkuu katika mpango huo) na wenzake waliotajwa kwa kutumia mkakati uliotajwa walitaka kuwapindua viongozi waliopo madarakani kwa utaratibu usiofaa wa kuwachafua kituhuma jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya Chadema.
“…Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni mpango wa kuipasua CHADEMA na kuiangamiza kabisa kwenye uso wa siasa za Tanzania. Huu sio mkakati wa kufanya mabadiliko ya kiuongozi ndani ya chama kwa njia za kidemokrasia na za kikatiba. Ni mpango wa kukiteka nyara chama na kukiua,” ilisema taarifa hiyo ambayo dev.kisakuzi.com ina nakala yake.
Hata hivyo taarifa hiyo imesema Zitto pamoja na Dk. Mkumbo walikili kwenye kikao cha Kamati Kuu na kuomba wao wahusika katika mpango huo wajiuzulu wenyewe nafasi zao, lakini Kamati Kuu ilipinga na kuona haja ya kuwavua uongozi moja kwa moja kama adhabu ya awali.
“…Mkakati wa Mabadiliko 2013 umejaa kashfa kubwa, matusi mengi na udhalilishaji mkubwa wa chama, viongozi wake wakuu na wanachama kwa ujumla. Kwa mfano Mwenyekiti wa Chama Taifa ametuhumiwa na wanaMtandao hawa kuwa ni mtu mwenye uzalendo unaotia shaka, mwenye elimu ya magumashi, mzito kujieleza, mtu mwenye akili ndogo na mengine mengi,”
“..Hivyo basi Kamati Kuu ya Chadema katika kikao chake tajwa kwa mamlaka iliyopewa kikatiba ya dharura chini ya ibara ya 6.5.2(d) ya Katiba ya Chama, imeadhimia yafuatayo; Kwamba, kuanzia sasa, viongozi wote waliohusika ama kuhusishwa na mkakati huu, yaani Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe, Mjumbe wa Kamati Kuu Dk Kitilla Mkumbo na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha Samson Mwigamba wavuliwe nyazifa zao zote za uongozi ndani ya chama,”
“Kwamba kamati ya chama ya Wabunge inaelekezwa kuchukua hatua za haraka za kuhakikisha Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe anavuliwa madaraka yake yote kama Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, with immediate effect;,” ilisema baadhi ya taarifa hiyo.
Aidha Kamati Kuu imeunda timu ndogo ya pamoja ya watendaji toka sekretarieti ya makao makuu na wajumbe wa Kamati Kuu ambayo itafanya kazi ya kuchunguza kumbaini muhusika mwingine aliyekuwa akituhumiwa kuhusika na kundi la akina Zitto ili naye achukuliwe hatua mara moja.
“…Tunawaomba Watanzania, wanachama na viongozi watu wasife moyo, bali waendelee kukiunga mkono chama chao cha ukombozi. Tunawaomba Watanzania, wanachama na viongozi wetu waendelee kulilinda tumaini lao pekee la mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu,” ilisema taarifa hiyo.