Sababu ya kujiuzulu kwa kocha Capello!

Aliyekuwa Kocha Mkuu wa England, Fabio Capello

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Uingereza (England), muitalia, Fabio Capello amejiuzulu rasmi kuifundisha timu hiyo. Capello amefikia hatua hiyo jana baada ya kufanya mkutano wa takribani saa nzima na viongozi wakuu wa Chama Cha Soka cha Uingereza (FA).

Mkutano huo uliowahusisha Mwenyekiti wa FA, David Bernstein, Katibu Mkuu wake, Alex Horne pamoja na Capello mwenyewe ulikuwa ukijadili sakata la kuondolewa kwa mchezaji wa Chelsea, John Terry katika nafasi ya unahodha kwenye timu ya Taifa ya Uingereza.

Chama cha FA kiliamuwa kumvua nafasi ya unahodha, Terry baada ya tuhuma za kumtusi kiubaguzi, mchezaji Anton Ferdinand uamuzi ambao haukumpendeza Capello kwa kile kutohusishwa na adhabu hiyo.

Capello, mwenye umri wa miaka 65, alieleza wazi kwenye moja ya televisheni kuwa hakupendezwa na uamuzi wa FA uliofanywa bila yeye kushirikishwa. Hata hivyo tayari FA imeridhia ombi la kujiuzulu kwa kocha Capello.

“Tumekubali ombi la kujiuzulu kwa Capello, nakubali huu ni uamuzi sahihi dhidi yake. Tunamshukuru sana kwa mchango wake kwa timu ya England na kunamtakia mafanikio mema anakokwenda,” alisema Bernstein.

Capello alisaini kuanza kuifundisha timu ya Uingereza Januari 2008 baada ya timu hiyo kufanya vibaya chini ya Kocha, Steve McClaren.