Na Janeth Mushi, Arusha
JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia watu saba wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, ambao walikutwa na bunduki mbili moja ikiwa ni SMG iliyokuwa na risasi 27 pamoja na bastola yenye risasi 4.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Thobias Andengenye alisema watuhumiwa hao wamekamatwa Agosti 17 na 18 mwaka huu. Andengenya alisema watuhumiwa hao walikuwa wamepanga njama kupora fedha zilizokuwa zikipelekwa benki za kampuni ya Bulk ya jijini hapa.
Alisema baada ya mtego wa polisi walifanikiwa kuwakamata majambazi hao kabla hawajafanya uporaji, ambapo uchunguzi wa awali unaonesha watuhumiwa wamehusika na matukio ya ujambazi katika Wilaya ya Rombo, Kilimanjaro.
Andengenye alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo ya Olmatejoo na Sanawari ya Juu wanadaiwa kufanya vitendo vya uhalifu katika wilaya ya Arusha kwa siku za nyuma. Aliwataja kuwa ni Yayaha Suleiman maarufu kwa jina la Jam (39) mfanyabiashara wa Olmatejoo, Philemon Inyasi (44) mkazi wa Kiboriloni Moshi.
Wengine ni pamoja an Frank Njau (35), fundi simu, mkazi wa Kambi ya Fisi Arusha, Frank Mollel (35), Charles George (40) wote wakazi wa Sanawari. Wengine ni Priva Kawishe (29) Tarakea na Julius Mtana (29) Tarakea ambapo wanendelea kuhojiwa kuhusiana na makosa ya mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Kwa mujibu wa Andengenye baadhi ya watuhumiwa hao wa ujambazi wamebainika kuwa wametoka jela hivi karibuni kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.