Saba Wafariki Baada ya Mabasi Kugongana Wilayani Bunda

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara Kamishina Msaidizi, Absalom Mwakyoma

WATU saba wamefariki dunia na wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa kufuatia mabasi mawili kugongana uso kwa uso katika Kijiji cha Nyatwali Wilayani Bunda Mkoani Mara.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara Kamishina Msaidizi, Absalom Mwakyoma alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11 jioni ikihusisha mabasi mawili ya Mwanza Coach lenye namba za usajili T 756 AWT aina ya scania marcopolo mali ya Halfan Ahmed wa mwanza likitoka Musoma kuelekea Mwanza pamoja na basi la Bestline lenye namba T 535 AJR lililokuwa likitokea Mwanza kuelekea Sirari.

Mwakyoma alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa mabasi hayo na madereva kutokuwa makini ambapo yalifika katika eneo la barabara ambayo inafanyiwa ukarabati na kupita kwa mwendo kasi.

“Madereva wa mabasi yote mawili walikuwa katika mwendo kasi katika barabara ya vumbi inayofanyiwa ukarabati na hawakuweza kuonana na kusababisha kugongana uso kwa uso na kupelekea vifo vya watu saba na zaidi ya 40 kujeruhiwa.

“Watu sita walifariki palepele katika eneo la ajali na mtu mmoja alifariki muda mchache baada ya kufikishwa katika Hospitali teule ya Wilaya ya Bunda DDH,” alisema kamanda Mwakyoma.

Kamanda Mwakyoma alisema majeruhi wa ajali hiyo wamelezwa katika Hospitali ya DDH na kati yao wanne kati 14 ambao walikuwa hawajitambui wamepelekwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi kwani hali zao sio nzuri kutokana na kuvuja damu nyingi na hivyo hospitali ya wilaya ya bunda kutokidhi mahitaji ya damu.

Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda na kuwaomba Wananchi kwenda kuitambua.

“Madereva wote wawili wamekimbia mara baada ya kutokea kwa ajali hiyo lakini kila siku tumeendelea kuwahelimisha madereva juu ya mwendo kasi lakini bado wapo madereva wasiokuwa makini na tutaendelea kuwachukulia hatua kali wale wote wana kaidi.

“Lakini abiria nao inabidi wasaidie katika hili wanapoona madereva wanakwenda mwendo kasi mara wamzue na mara waonapo askari wa usalama barabarani watoe taarifa,”alisema Mwakyoma.

Baadhi ya abiria walikuwemo kwenye mabasi hayo walisema kuwa mabasi hayo yalikuwa na mwendo mkali ambapo walijaribu kupiga kelele kuwaambia madereva kupunguza mwendo lakini hawakuweza kusikilizwa na muda mfupi ajali ikatokea.

Walisema kuwa ni vema sasa Serikali ikachukua hatua kali kwa madereva wazembe ili kuzinusuru roho za watu ambao ni nguvu kazi ya taifa ambazo zinateketezwa kwa uzembe wa madereva.

Hii inakuwa nia ajali ya pili ya mabasi ya abilia kutokea katika barabara ya Musoma kwenda Mwanza ndani ya wiki mbili baada ya kutokea ajali nyingine ya basi la Bunda Expless likitopkea Wilayani Bunda kuelekea Mtukula.

CHANZO: www.shommibinda.blogspot.com