Rwanda yashambuliwa

Rais wa Rwanda, Paul Kagame

TAKRIBAN watu 18 wamejeruhiwa vibaya kufuatia shambulio la gurunedi lililofanyika mjini Kigali. Maofisa wa polisi wamesema hakuna mtu aliyeuawa katika shambulio hilo lilofanyika usiku wa Jumanne.

Taarifa zinasema bado haijafahamika waliohusika na shambulio hilo, na tayari upelelezi umeanza. Mwanamke mmoja aliiambia BBC kuwa; “Nilikuwa nakwenda kuchukua simu yangu nikasikia mlipuko mkubwa, tukaanguka hapa na pale, wengi walinilalia wale waliokuwa nyuma yangu ndio waliojeruhiwa vibaya sana,” amesema.

Mwanamke huyo anasema kulikuwa watu wengi katika eneo la tukio na wengi wamejeruhiwa vibaya na kwamba wengine walipekelekwa hospitalini wakiwa hali mahututi. Shambulio hilo limetokea katika soko moja katika eneo la Gasambo, mjini Kigali, lenye msongamano mkubwa wa watu.

Shambulio hilo limetokea mwaka mmoja baada ya mfululizo wa mashambulio ya magurunedi yaliyokumba mji wa Kigali, ambapo washukiwa 30 walifikishwa mahakamani.
-BBC