Mwandishi Maalumu, Nairobi
SERA ya Serikali ya Tanzania kutoa ruzuku ya mbegu na mbolea kwa wakulima wadogo wadogo wa chakula nchini imeanza kuzaa matunda kwa maana ya kuwepo kwa ongezeko kubwa la uzalishaji wa chakula na hasa mahindi nchini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameuambia mkutano wa kimataifa.
Aidha, Rais Kikwete ameitaka Jumuia ya Kimataifa kutimiza wajibu wake wa kihistoria kuzisaidia nchi masikini zinapokabiliwa na baa la njaa ambalo linatokana na sababu zilizoko nje ya uwezo wa nchi hizo ukiwamo ukame na mabadiliko ya tabia nchi.
Rais Kikwete ameyasema hayo mjini Nairobi, Kenya, Septemba 9, 2011, wakati aliposhiriki na kuhutubia mkutano wa kimataifa uliojadili njia za kupata ufumbuzi wa muda mfupi wa kukabiliana na baa la njaa linalozikumba nchi za pembe la Afrika na njia za muda mrefu za kuepukana na baa hilo katika siku zijazo.
Rais Kikwete aliwasili mjini Nairobi Alhamisi jioni kuhudhuria mkutano huo wa siku mbili ambao leo umefanyika kwenye ngazi ya wakuu wa nchi na Serikali na ameungana na mwenyeji wa mkutano huo, Rais Mwai Kibaki wa Kenya, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, Rais Sheikh Sharif Sheikh Ahmed wa Somalia, Waziri Mkuu wa Ethiopia pamoja na wawakilishi wa nchi nyingi za Afrika na nje ya Afrika kushiriki katika mkutano huo.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais Kikwete amewaelezea wajumbe uzoefu wa Tanzania katika kujaribu kukabiliana na ukosefu wa chakula na kukomesha njaa ambako amesema kuwa moja ya njia zinazotumiwa na Serikali yake ni kutoa ruzuku kwa wakulima wadogo wadogo ili kuwaongezea uwezo wa uzalishaji.
“Ukosefu wa usalama katika upatikanaji wa chakula unaoyakabili mataifa yetu, ni matokeo kimsingi ya uzalishaji duni katika kilimo chetu. Kilimo chetu kwa kiwango kikubwa kimo mikononi mwa wakulima wadogo wadogo wa kujikimu ambao hawatumii teknolojia ya kisasa ama njia za kisayansi za uzalishaji. Katika hali hiyo, tunahitaji kuwasaidia kukabiliana na matatizo yanayopunguza uzalishaji wa chakula, “amesema Mheshimiwa Rais Kikwete.
Ameongeza: “Ni ukweli usiopingika kuwa pamoja na hali ya ukame, katika nchi zetu zote hizi yako maeneo ambako mvua ni nzuri kwa wastani na maeneo yenye maji mengi kutokana na mito, maziwa ama maji ya ardhini. Tutumie maeneo haya kupunguza athari za ukame na ukosefu wa chakula.”
“Sisi katika Tanzania tumekuwa tunafanya hivyo na zipo dalili nzuri za mafanikio. Tuna mikoa sita yenye mvua ya uhakika katika Tanzania Bara. Tumeiteua hii kuwa ndiyo ya kuilisha nchi yetu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Tumepitisha sera ya Serikali ya kuwasaidia wakulima kwa mbegu, mbolea, dawa na mahitaji mengine ya kilimo katika mikoa hiyo. Baadaye tulianzisha ruzuku kwa mbegu na mbolea. Hili limetusaidia sana. Uzalishaji umeongezeka na mikoa hii sasa inazalisha chakula cha ziada kinachoilisha mikoa mingine inayokihitaji na kingine hata kuzuka mipaka ya nchi yetu.”
Kuhusu misaada ya Jumuia ya Kimataifa wakati wa ukosefu wa chakula kwa nchi masikini, Rais Kikwete amesema: “Serikali zetu zinajitahidi. Lakini kwa sababu ni Serikali za nchi masikini, Jumuia ya Kimataifa inao wajibu wa kihistoria kutusaidia ambako jitihada zetu zinakomea na hatuwezi kupambana peke yetu. Na misaada yao inatakiwa iwe ya kutosha na itolewe kwa wakati.”
Mkutano huo kwenye eneo la Umoja wa Mataifa nje kidogo ya mji wa Nairobi umekuwa ni mkutano muhimu kwa nchi za Pembe ya Afrika. Inakadiriwa kuwa kiasi cha watu milioni 12 wanahitaji msaada wa chakula cha dharura katika nchi za Kenya, Somalia, Djibouti na Ethiopia ambazo kwa pamoja zinakabiliwa na hali ya ukame ambayo haijapata kutokea katika eneo hilo katika miaka 20 iliyopita tokea mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Nchi ya Somalia ambayo imekuwa inakabiliwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya miongo miwili ndiyo imeathirika zaidi ikiwa inakadiriwa kuwa kiasi cha watu 3.7 milioni nchini humo wanakabiliwa na baa la njaa.
Majimbo yaliyoathirika zaidi ni ya Shebelle Chini na Bakool na kuwa kiasi cha watu 2,500 wanapoteza maisha yao kila siku mbali na kuwa kiasi cha Wasomali 1,300 wanaokimbia nchi yao kuingia Kenya kila siku, 8,000 wanaoingia Ethiopia kila mwezi na wakimbizi 17,000 ambao wako tayari nchini Djibouti.
Idadi ya wananchi wa Djibouti wanaohitaji chakula na misaada ya haraka ya dharura ni kiasi cha 120,000 na kiasi kikubwa cha mifugo kimeathirika katika nchi hiyo kutokana na mvua za shaka sana katika misimu miwili iliyopita.
Kiasi cha watu milioni 4.5 wanahitaji misaada ya kibinadamu katika Ethiopia na hasa katika mikoa ya Somalia na Oromia. Kwa sababu ya ukame katika mikoa hiyo na mikoa mingine ya Ethiopia, inakadiriwa kuwa kiasi cha wanafunzi 60,000 wamelazimika kuacha shule.
Katika Kenya, idadi ya watu walioathirika kwa kukumbwa na ukame na njaa wanakadiriwa kufikia milioni 3.7 wakiwemo wakimbizi 477,000 kutoka Somalia. Bei ya nafaka nchini Kenya imeongezeka kwa asilimia 160 katika mwaka mmoja uliopita na wafugaji nchini humo wanalazimika kuuza mbuzi watano kwa sasa kuweza kupata kiroba cha kilo 90 za mahindi ikilinganishwa na mbuzi mmoja ama wawili mwanzoni mwa mwaka huu.
Tathmini za kimataifa zinabainisha kuwa mahitaji ya misaada ya kibinadamu kwa nchi hizo za Pembe ya Afrika zilizoathirika na ukame na njaa ni kiasi cha dola za Marekani bilioni 2.5. Mpaka sasa kiasi kilichopatikana ni dola za Marekani bilioni 1.4 ambayo ni sawa na asilimia 58 ya mahitaji.
Mpaka Tanzania imekwishakutangaza kutoa msaada wa tani 300 za mahindi kwa Somalia na pia kuchangia kiasi cha dola 200,000 katika mfuko wa kuchangia mahitaji na fedha taslimu katika mfuko wa kuzisaidia nchi za Pembe ya Afrika.
Hata hivyo, mkutano wa leo haukuwa wa kuchangisha fedha kwa ajili ya nchi zilizoathiriwa na ukame. Badala yake, mkutano huo unalenga kuweka mikakati ya jumla ya kikanda katika kupambana na ukame wa mara kwa mara katika eneo hilo na ambao unaweza kusababisha madhara makubwa zaidi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa usalama.