Kiongozi wa kanisa Katoliki Dunia Papa Benedict amesema matumizi ya mipira ya kiume inaweza kuhalalishwa kutokana na hali ilivyo, ili kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya HIV/UKIMWI. Matamshi hayo yanayotarajiwa kuchapishwa katika kitabu wiki ijayo, yanaashiria kulegeza msimamo wake mkali wa zamani dhidi ya matumizi wa kondomu kupambana na HIV. Vatikana kwa muda mrefu imekuwa ikipinga matumizi ya kondomu, kama njia ya kupanga uzazi. Hatua hiyo ilizua shutuma kali, hasa kutoka kwa wanaharakati wa kupambana na UKIMWI, ambao wanasema kondomu ni moja ya njia ambazo zimethibitishwa katika kupambana na maambukizi ya HIV. Papa Benedikt katika ziara yake nchini Cameroon mwaka jana alisema kugawa kondomu kunaweza kuchochea maambukizi ya HIV, matamshi ambayo yalizua shutuma kutoka kwa nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya. Hata hivyo, katika matamshi yake ya hivi karibuni, Papa amesema matumizi wa kondomu yanaweza kuhalalishwa katika mazingira fulani ya kipekee. Ametoa mfano wa makahaba wa kiume, ambapo amesema matumizi ya kondomu kuzuia maambukizi ya UKIMWI yanaweza kuonekana kama kitendo cha mtu kuwa na majumuku, ingawa amesema kondomu “sio njia halisi ya kupambana na uovu wa kuambukiza HIV”.
(WWW.BBCSWAHILI.COM)