MAMLAKA ya Uendeshaji wa Bonde la Mto wa Rufiji (RUBADA) jana ilitia saini mkataba wa uzalishaji wa umeme na Kampuni ya Sinohydro ya nchini China kwa ajili ya kuzalisha umeme katika eneo la Mpanga, lililopo ndani ya Bonde la Kilombero.
Akizungumza katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa RUBADA, Aloyce Masanja, alisema mradi huo utaanza hivi karibuni na kwamba utazalisha kiasi cha megawati 165.
“Baada ya kutiliana saini leo, hawa wenzetu watakwenda kufanya majumuisho ya mwisho na kazi itaanza mapema kwani suala la fedha tayari tumeshazungumza na Benki ya Exim nchini China na wamekubali kutukopesha kwa ajili ya mradi huu.
“Mradi huo utaendeshwa kwa ushirikiano na kampuni hiyo kwa muda wa miaka mitano na baada ya hapo utakabidhiwa kwa watu wa RUBADA ili wauendeshe wao.
“Huu utakuwa ni mradi wa miaka mitano kwa maana kwamba kwa kipindi hicho tutakuwa pamoja na hawa wenzetu wakitufundisha jinsi ya kuuendesha pia watu wetu baadhi watakwenda China kwa ajili ya kupata mafunzo zaidi,” alisema Masanja.
Alisema tayari Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeonyesha nia ya kununua umeme huo na kuuingiza kwenye gridi yake.
source: Gazeti la Mtanzania