MABALOZI wa Usalama Barabarani nchini Tanzania (Road Safety Ambasadors-RSA) wamekabidhi misaada kwenye Ofisi ya Kitengo cha Mawasiliano cha Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi nchini (Traffic Control Center-TCC).
Vifaa hivyo ambavyo ni vitendea kazi katika kituo cha taarifa cha Kitengo cha Mawasiliano cha Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi nchini, vimekabidhiwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa RSA, John Seka ikiwa ni michango ya mabalozi hao.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kukabidhi, Seka alisema lengo la msaada huo ni wa Mabalozi wa Usalama Barabarani ni kutaka kuboresha mawasiliano ya Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani.
Alivitaja vifaa vilivyokabidhiwa kuwa ni pamoja na Radio mbili za mawasiliano za kidijitali, Simu ya mawasiliano aina ya Tablet iliyounganishwa na makundi ya RSA ya Facebook, Whatsapp na Telegram, Mtungi wa Maji ya Kunywa, Viti vya kukalia, Feni na Zulia la Ofisi ya TCC.
Aidha Seka alitaja msaada mwingine ni Birika la kuchemsha maji ya chai, Mfumo wa kutunza betri kwa ajili ya Tablet (Power Bank) na Gharama za Upakaji wa Rangi wa ofisi ya TCC ikiwa vyote vinalenga kuhakikisha ofisi ya TCC inafanya kazi kwa ufanisi na bila vikwazo ili kurahisisha mawasiliano kati ya RSA na TCC.
“RSA ni mkusanyiko wa watanzania wanaotumia mitandao ya kijamii yaani Social Media katika mawasiliano. Hawa ni Watanzania wanaoamini kuwa mitandao ya kijamii ya Facebook, Whatsap na Telegram inaweza kutumiwa kuleta mabadiliko katika jamii. Huu ni mtazamo chanya ulio na lengo la kuhakikisha kuwa tunabadili mtazamo wa kuwa mitandao ya kijamii inatumika vibaya,” alisema Seka akifafanua juu ya RSA.
Aliongeza kuwa RSA ilitambulishwa rasmi tarehe 17 October 2013 na kuzinduliwa rasmi tarehe 28 Desemba 2014 katika ukumbi wa bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay na hadi sasa ina zaidi ya wananchama 5000 walioko Facebook, wanachama 500 katika group la Whatsapp la kitaifa na yale ya mikoani na pia wanachama 400 wako Telegram.
“…Kinachofanywa na RSA ni kuhakikisha kuwa tunawapa watanzania ujasiri wa kuripoti matukio ya uvunjifu wa sheria na kanuni zinazoratibu usalama wa watanzania wakiwa barabarani. Kwa kutumia simu zao wanaRSA hupiga picha za matukio ya uvunjifu wa sheria za barabarani na kuzituma kwenye haya magroup niliyoyaelezea hapo juu.” Alisema Mwenyekiti huyo wa RSA katika taarifa yake.
*Taarifa hii imeandaliwa na www.thehabari.com