*Yasaidia kumwokoa msichana aliyetaka kubakwa
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Dhamiri Kidavashari ameamua kutangaza namba yake kwa wakazi wa wilaya mpya ya Mlele, mkoani humo. RPC Kidavashari ambaye anafuatana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwenye ziara yake ya jimbo la Katavi, wilayani Mlele, ametumia fursa ya utambulisho kwa wananchi kwa kutangaza namba yake ambayo ni 0769-168-850 ili wananchi wampatie taarifa kuhusu matukio ya uhalifu.
Aliwaeleza wananchi katika kata na vijiji mbalimbali ambavyo Waziri Mkuu amepitia kwamba ulinzi wa nchi na uwepo wa amani unategemea ushiriki wa wananchi na kwamba suala hilo si la polisi peke yake. Aliwasihi wawe wepesi kutoa taarifa pale wanapohisi kuna jambo ambalo si la kawaida.
Katika mahojiano maalum, Desemba 18, 2012, Afande Kidavashari alisema uamuzi wake wa kutangaza namba ya simu ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya polisi jamii ambayo inatekelezwa Kitaifa.
“Sasa hivi hata ukiingia kwenye mabasi, utakuta namba za Makamanda wa Polisi wa Mikoa zimebandikwa ndani ya mabasi ikiwa ni njia ya kupunguza ukiritimba wa kupokea taarifa kutoka kwa wananchi…pia ni njia ya kuturahisishia mawasiliano na kutuweka karibu na wananchi,” alisema.
Alipoulizwa kama hatua yake hiyo imeleta manufaa yoyote, Afande Kidavashari alikiri kupokea taarifa zilizosaidia binti mmoja asibakwe na vijana wa bodaboda mwishoni mwa wiki iliyopita. “Kuna raia mwema aliona vijana wakimvamia binti mmoja katika eneo moja hapa Mpanda, akanipigia simu, nikatuma askari ambao waliwahi katika eneo la tukio na kumwokoa yule msichana. Vijana wawili walikamatwa na mmoja alikimbia, bado tunamfuatilia,” alisema.
Akitoa mfano mwingine, afande huyo alisema kuna meseji (sms) aliipokea kutoka Ugalla mara baada ya Waziri Mkuu kufanya mkutano katika kata hiyo ambapo kuna mkazi mmoja alionewa na watu wa Kaliua. “Mimi niliituma ile sms kwa RPC Tabora naye akaituma kwa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kaliua (OCD) na wameniarifu kuwa suala hilo tayari limeanza kushughulikiwa,” aliongeza.
Akizungumzia aina ya matukio ya uhalifu yanayotokea mara kwa mara mkoani humo, Kamanda huyo wa polisi alisema mengi ni ya uhamiaji haramu, uvuvi haramu, wizi wa ng’ombe, wizi wa mbao kwenye misitu ya hifadhi na uingizaji wa silaha haramu.