Na Mwandishi Wetu, Rombo
SIKU chache baada ya kuripotiwa kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya nguruwe wilayani Rombo, baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo wameiomba Serikali kuhakikisha inatoa elimu zaidi juu ya maambukizi ya ugonjwa huo ili kudhibiti maambukizi zaidi.
Kauli hiyo imetolewa mjini hapa kwa nyakati tofauti na wananchi huku wakisisitiza kuwa ipo haja kwa Serikali kupitia wataalamu wake kutoa elimu kutokana na ukweli kwamba wananchi wengi hawana uelewa kuhusu namna ugonjwa huo unavyoambukizwa na athari zake kwa binadamu.
“Kuna watu hapa wanachinja mizoga ya nguruwe wanakula na hata kuwauzia watu, hii ni dhahiri kuwa hawajui madhara yake,” alisema Hermani Massawe Mkazi wa Usseri.
Hata hivyo wananchi pia wameitupia lawama serikali kwa kitendo cha kushindwa kupeleka wataalamu wa mifugo maeneo ya vijijini ili watoe chanjo ya ugonjwa huo. Mmoja wa wakazi wa Usseri, Daria Pius aliongeza kuwa wanashangaa kuona wataalamu wa mifugo wakiishia maeneo ya mijini tu huku maeneo ya vijijini kusahaulika wakati ndio wahitaji wakubwa wa huduma hizo.