Roho za Watanzania zaendelea kuteketea
*Ajali mbaya yaua tena 9, yajeruhi wengine
Na Joachim Mushi
IKIWA ni siku chache tangu ajali ya wasanii wa kundi la five star kutokea Mkoa wa Morogoro na kuua wasanii 13 wa kundi hilo na nyingine kutokea tena eneo jirani na lile na kuua watu watatu na wengine kujeruhiwa, imetokea nyingine mbaya na kuua watu tisa.
Kwa mujibu wa taarifa tulizozipata muda huu kutoka kwa shuhuda ambaye yupo safarini eneo hilo, gari aina ya coaster namba T 566 AZP lililokuwa likitoka Chalinze kwenda Dar es Salaam limegongana na lori namba T 535 AAG; na imedaiwa watu tisa wamekufa papo hapo na wengine kujeruhiwa vibaya.
Akizungumza na shuhuda huyo amesema coaster ililikuta lori limesimama njiani na likitaka kulipita lilitokea lori lingine mbele ndipo dereva alipoamua kulivamia lori lililosimama akijaribu kukwepa kugongana uso kwa uso na lori la mbele yake.
Shuhuda huyo amesema kuwa waliokufa wote wametoka kwenye coaster na maiti zinaondolewa na inadaiwa zinapelekwa hospitali ya Tumbi, Kibaha.
“Ajali hii imehusisha gari aina ya coaster ambalo lilikuwa likitokea Chalinze kwenda Dar es Salaam, limegongana na lori lenye tela dereva wa coaster inaonekana kavunjika miguu yote…na gari imebondeka vibaya mbele..,” anasema na kuendelea.
“Hapa kwa sasa magari hayatembei maana ajali imeziba barabara foleni ni ndefu kuanzia maeneo ya Daraja la Ruvu hadi eneo la ajali,” alisema shuhuda huyo liyejitaja kwa jina moja la Ally akizungumza kwa njia ya simu The Habari.Com.
Aidha alisema eneo ilipotokea ajali ni kilomita chache kabla ya kufika Kiluvya ukitokea Chalinze majira ya saa tano na tayari askari wa usalama barabarani wamefika kutoa msaada kwa wahusika, huku wakijitahidi kuongoza magari kwani barabara ilifungwa na ajali hiyo.
Tunaendelea kukusanya taarifa na tutawaleteeni kadri zinavyotufikia kutoka kwa vyanzo vya THE HABARI.COM.