Robin van Persie mchezaji bora wa mwaka 2012

Robin van Persie katika moja ya hekaheka uwanjani

Robin van Persie amechaguliwa mchezaji bora wa mwaka katika tuzo inayotolewa na Chama cha Wacheza Kandanda ya Kulipwa- PFA.
Mshambuliaji huyo wa Arsenal mwenye umri wa miakan 28 ameshapachika mabao mara 38 msimu huu, yakiwemo mabao 34 aliyoifungia Arsenal katika mashindano yote.
Mchezaji huyo ambaye pia huchezea timu ya taifa ya Uholanzi, akiwa anaongoza kwa kufunga mabao msimu huu wa ligi ya England alisema: “Iwapo watu wanasema hivyo, ni jambo maalum sana, lakini linakuwa maalum zaidi iwapo hata wapinzani wako wanalizungumza.
“Iwapo wamekusanya mawazo yao na kukiri mimi ni mchezaji bora basi ni heshima kubwa hiyo.”
Van Persie, ambaye amekuwa kichocheo cha ushindi kwa kikosi cha Arsene Wenger, haraka alielezea umuhimu wa wachezaji wenzake wa Arsenal.
“Bila ya wao nisingefikia mafanikio yote haya,” alisema. “Mathalan, Theo Walcott, amenipatia zaidi ya pasi 12 na kwa kweli namshukuru sana.
Van Persie msimu huu mambo yake yamekuwa safi tangu alipojiunga na Arsenal mwaka 2004, akiwa ameisaidia kwa kiasi kikubwa safu ya ushambuliaji wa kati.
“Kusema haki, mara ya kwanza nilipojiunga na Arsenal sikuwa najiamini na sikuwa na hakika kama nitafanya mambo makubwa,” aliongeza kusema.
“Ilinichukua muda kiasi lakini baada ya miezi michache polepole nikaanza kujiamini kwamba naweza kufanya kazi nzuri ndani ya Arsenal.”
Van Persie ameshinda tuzo hiyo akiwatangulia Wayne Rooney wa Manchester United, Scott Parker wa Tottenham na wachezaji watatu wa Manchester City Sergio Aguero, Joe Hart na David Silva.
Mlinzi wa Tottenham na timu ya taifa ya England Kyle Walker ameshinda tuzo ya PFA ya mchezaji bora Kijana wa Mwaka.
Manchester City ndio ilikuwa na wachezaji wengi waliowania tuzo hiyo ya mwaka. Walifanikiwa kuwa na wachezaji wanne – Joe Hart, Vincent Kompany, David Silva na Yaya Toure.

-BBC