RITA na Mafanikio ya Mkakati wa Usajili wa Utoaji wa Vyeti vya Kuzaliwa

birth_certificate

Na Benedict Liwenga, Maelezo-DSM.

MOJA YA MAJUKUMU makubwa  ya Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kama taasisi ya Serikali iliyopo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria ni kuratibu na kusimamia usajili wa vizazi na vifo nchini.

Cheti cha kuzaliwa hutolewa kwa mwananchi mara baada ya kusajiliwa kwani cheti hicho ni nyaraka muhimu na kisheria ndiyo pekee inayotakiwa kuthibitisha tarehe ya kuzaliwa, mahali alipozaliwa na wazazi wa mmiliki wa cheti hicho.

Mnamo mwezi Aprili, 2014, RITA ilizindua Mkakati wa kusajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa wananfunzi wa shule za Msingi pamoja na Sekondari katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Malengo makuu ya mkakati huo yalikuwa ni kusogeza huduma karibu na wananchi kwani badala ya wanafunzi au wazazi ama walezi kufuata huduma za usajili katika Ofisi za RITA, mkakati huo urahisisha kwani unawafanya waweze kupata veti hivyo katika shule anayosoma mtoto.

Dhumuni la pili la mkakati huo ni kuwapatia wanafunzi haki yao ya msingi ya kuwa na utambulisho wa nasaba kupitia cheti cha kuzaliwa, kuwapa wanafunzi hao uelewa wa kina kuhusu umuhimu wa kuwa na cheti cha kuzaliwa pamoja na kuwawezesha wanafunzi kuwa na cheti cha kuzaliwa ambacho watakitumia pale kinapohitajika.

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Masoko, Mawasiliano na Elimu kwa Umma ya RITA, katika mkakati huo, kila shule imeteua mwalimu mmoja ambaye jukumu lake ni kuratibu usajili katika shule yake baada ya kupewa mafunzo maalum ya kina kuhusu usajili wa vizazi.
Mwalimu huyo huwapa fomu za maombi wanafunzi ambao hawana vyeti vya kuzaliwa ambapo fomu hizo hujazwa na wazazi au walezi wao na kasha hurejeshwa kwa walimu hao zikiwa na viambatisho vinavyohitajika.

Kazi inayofuata baada ya kupokelewa fomu hizo ni ya uhakiki wa awali ambapo baada ya uhakiki huo kukamilika mwalimu huzipeleka RITA kwa uhakiki wa kina na hivyo basi vyeti huweza kuandaliwa kwa maombi yale yaliyokidhi vigezo baada ya shughuli ya vyeti kukamilika, hupelekwa kwa Mwalimu Mratibu ambaye yeye hivigawa kwa wanafunzi husika.

Moja ya mafanikio makubwa ya mkakati huo ni kwamba zaidi ya wanafunzi 15,120 wameweza kusajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa kati ya lengo la kusajili wanafunzi 21,000 wa Manispaa ya Ilala kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Taarifa inabainisha kuwa, kati ya hao waliosajiliwa, 7,712 ni wasichana na 7,408 ni wavulana.

Aidha, kupitia elimu inayotolewa na walimu, uelewa wa wanafunzi, wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa cheti cha kuzaliwa umeongezeka kwani wazazi wengi wameshawishika kufanya usajili na kupata vyeti kwa ajili ya familia nzima.

Baada ya Mkakati huo kufanikiwa katika Manispaa ya Ilala, RITA inatarajia kuanza kuueneza katika Manispaa na Wilaya nyingine za Tanzania Bara na kwa kuanzia itakuwa ni Manispaa ya Kinondoni pamoja na Manispaa ya Temeke mnamo mwezi Januari 2015.

Ikiwa ni wito kwa wazazi na walezi wote, ni vema wajitahidi kutumia fursa hiyo ya kuwapatia vyeti watoto wao wanaosoma katika shule ambazo program hiyo inatekelezwa kwani mkakati huo hutumia mfumo rahisi usio na usumbufu na wenye kupunguza gharama kwa wazazi na kubwa katika hilo mtoto anapata cheti halisi.

Programu hiyo inaendeshwa na RITA kwa kushirikiana na Idara za Elimu za Msingi na Sekondari katika Manispaa ya Ilala ambapo mkakati huo kwa sasa unaendelea katika jumla ya shule 201 ambapo 105 ni shule za Msingi na 96 ni za Sekondari.